Nafasi Ya Matangazo

September 03, 2026




Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju amewataka Naibu Wasajili wa Mahakama nchini kuendelea kutekeleza majukumu yao ipasavyo huku wakilinda maslahi ya haki (Interest of Justice).

Mhe. Masaju ameyasema hayo leo tarehe 31 Agosti, 2026 alipokuwa akifungua Mafunzo Elekezi kwa Naibu Wasajili wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

“Tuna wajibu wa kuendelea kutekeleza majukumu yetu kwa kulinda maslahi ya haki, kwa kutokufungwa kwa masharti ya kiufundi kupita kiasi hadi kukwamisha upatikanaji haki,” amesema Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju amesema kuwa, Wasajili wa Mahakama ndio 'injini' ya Mahakama. Hivyo, wana nafasi kubwa katika maendeleo ya Mhimili huo ambao mamlaka yake kwa mujibu wa Ibara ya 4 ni kutekeleza jukumu la utoaji haki.

“Kwa mujibu wa Ibara ya 107A(1), Mahakama ndio yenye kauli ya mwisho kwenye masuala ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano. Na ukiwa unaongozwa na kanuni kadhaa: mojawapo, kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kiuchumi au kijamii, kutochelewesha haki bila kuwepo sababu ya msingi na kwamba itakuwa huru, italazimika tu kuzingatia sheria za nchi na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama ambavyo Ibara ya 107A inavyoelekeza,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju amesema, shughuli zote za umma huongozwa na kusimamiwa na sheria; hakuna shughuli yoyote ya umma ambayo haiongozwi na kusimamiwa na sheria. Na kwa sababu hiyo, Katiba inakuwa pia sheria, kwa mujibu wa ile Sheria ya Tafsiri za Sheria, sura ya kwanza ya Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Jaji Mkuu amewakumbusha Naibu Wasajili hao kuwa waadilifu ili wanapofanya maamuzi, watu waone kweli kwamba haki imetendeka. Amesisitiza, “Na katika hilo lazima tuwe waadilifu, tunapoacha kuwa waadilifu, tukiwa wazembe, tukiwa wavivu, uwezo wetu ukiwa mdogo, watu hawatatuheshimu.”

Vilevile, Mhe. Masaju amekemea vikali tabia ya baadhi ya watu kuingilia uhuru na maamuzi ya Mahakama huku akibainisha kuwa, Katiba imeiwekea ulinzi kwa Mahakama kupitia Ibara ya 30(2)(c) inayoelekeza kuhakikisha utekelezaji wa hukumu au amri ya Mahakama iliyotolewa katika shauri lolote la madai au la jinai.

Aidha, Ibara ya 30(2)(d) inatamka kulinda heshima, haki na uhuru wa watu wengine au faragha ya watu wanaohusika katika shauri lolote mahakamani, kuzuia kutoa habari za siri, au kulinda heshima na uhuru wa Mahakama.

“Ni lazima hukumu na amri za Mahakama zitekelezwe, ni Mahakama gani hiyo inaweza ikafanya maamuzi halafu yasitekelezwe, halafu ikabaki kuwa Mahakama?” amehoji Jaji Mkuu.

Ameongeza kuwa, Katiba hiyo pia inaelekeza kwamba lazima Mahakama iheshimike; uhuru wake, mamlaka, na hadhi yake lazima vilindwe na viheshimiwe. Kwa hiyo, lazima kulinda sifa na haki au uhuru wa watu wengine, au maisha binafsi ya watu wanaohusika katika mashauri mahakamani, kuzuia kutoa habari za siri, kutunza heshima, mamlaka, na uhuru wa Mahakama.
Posted by MROKI On Thursday, September 03, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo