Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimekubaliana kuondoa jambo la 15 la Maliasili ya mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuta ya aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa, na gesi asilia katika orodha ya mambo ya Muungano.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa wakati akijibu swali la
Mbunge wa Mtambwe Mhe. Rashid Habib Ali Rashid aliyeuliza Serikali ina mpango
gani wa kuondoa suala la Mafuta na Gesi kwenye orodha ya Masuala ya Muungano.
Akiendelea kujibu swali hilo, Mhe. Kwagilwa alisema kwa
sasa, suala la Mafuta na Gesi Asilia linasimamiwa na kila upande ambapo SJMT
imetunga Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia ya Mwaka 2015 ambayo chini ya kifungu
cha 11 imeanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA -
Petroleum Upstream Regulatory Authority).
Aliongeza kuwa kwa upande wa Zanzibar, SMZ imetunga
Sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia, Namba 6 ya Mwaka
2016 iliyoanzisha Mamlaka ya Udhibiti, Utafutaji na Uendelezaji wa Mafuta na
Gesi Asilia (ZPRA – Zanzibar Petroleum Regulatory Authority) na Kampuni ya
Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC – Zanzibar Petroleum
Development Corporation).
“Mheshimiwa Naibu Spika Kwanza niungane na Mheshimiwa
mbunge ambaye amesema kwamba Baraza la Wawakilishi lilisharidhia na
lilishawasilisha kutaka suala hili liondolewe na ndio maana Baraza la
Wawakilishi limetunga sheria ya kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti na hivyo
linashughulikiwa katika kila upande hivyo halina hoja kinzani,” alifafanua
Kwagilwa.
Pamoja na hayo, kila ongezeko au kuondolewa kwa masuala
ya Muungano hupata nafasi ya kujadiliwa na kupata ridhaa ya Serikali zote mbili
ya SJMT na SMZ na kupitia mchakato mahususi wa kikatiba.
Mabadiliko husika hupitia katika Baraza la Wawakilishi na
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ibara ya 98(1) ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inaruhusu Bunge kutunga sheria kwa ajili
ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
lakini kwa utaratibu maalumu ufuatao ulioainishwa na Katiba.



.jpg)
.jpg)
.jpg)



0 comments:
Post a Comment