Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange
akijibu maswali bungeni wakati wa Kikao cha Saba cha Mkutano wa Pili wa Bunge
jijini Dodoma leo Februari 04, 2026.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad
Yussuf Masauni (kulia) akizungumza na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange wakati wa kipindi cha maswali
na majibu katika Kikao cha Saba cha Mkutano wa Pili wa Bunge jijini Dodoma leo
Februari 04, 2026. Mbele ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Mhe. Hamis Mwinjuma.
*******************
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema
katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025 jumla ya miradi kumi ya kuhifadhji
mazingira na kuhimili mabadiliko ya tabianchi yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 97.6 imetekelezwa na
kukamilika Zanzibar.Hayo yamebainishwa bungeni jijini Dodoma leo Februari
04, 2026 na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.
Dkt. Festo Dugange wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtambwe Mhe. Rashid Habib
Ali aliyetaka kufahamu Zanzibar inanufaikaje na fedha za mazingira zinazotolewa
na wafadhili.
Mhe. Dkt. Dugange ameliarifu Bunge kuwa utekelezaji wa
miradi ya mazingira umeleta manufaa kwa jamii kwa kuongeza kipato kupitia
shughuli mbadala hivyo kuongeza uwezo wa jamii katika uhifadhi wa mazingira na
kuhimili mabadiliko ya tabianchi
Akiendelea kujibu swali la mbunge huyo alifafanua kuwa
utekelezaji wa miradi hiyo umechangia katika ukuaji wa uchumi kwa maendeleo
endelevu na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Mhe. Dkt. Dugange alisema Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania imekuwa ikipokea fedha kutoka kwenye Mifuko ya Kimataifa ya Mazingira
na Mabadiliko ya Tabianchi na wafadhili mbalimbali wakiwemo Mfuko wa Mazingira
wa Dunia (GEF), Mfuko wa Mabadiliko ya tabianchi (GCF), Benki ya Dunia (WB) na
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Aidha, alibainisha kuwa fedha zinazopatikana zimekuwa
zikitumika kutekeleza miradi mbalimbali ya hifadhi ya mazingira na mabadiliko
ya tabianchi kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Hivyo, alisema Serikali imeendelea kuandaa miradi kwa
ajili ya kutafuta fedha kupitia vyanzo mbalimbali ambapo hadi sasa jumla ya miradi
mitatu yenye thamani ya takribani shilingi
bilioni 62.6 ipo kwenye hatua za awali za maandalizi.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri alisema fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
mazingira zinagawanywa kwa kuzingatia uwiano wa uhjtaji wa pande zote mbili za
Muungano.
Alisema mkakati wa Serikali
ni kuboresha maeneo yaliyoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi hususan ya kwenye
fukwe za bahari ambako maji huingia kwenye makazi ya wananchi na kuleta
madhara.
Mhe. Dkt. Dugange alisema
hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mhe. Ali aliyeuliza ni upi mgawanyo wa
utekelezaji wa miradi Tanzania Bara na Zanzibar.









0 comments:
Post a Comment