WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa ahadi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zimeendelea kutekelezwa kikamilifu ikiwemo ya kugharimia kwa asilimia 100 matibabu ya vipimo vya kibingwa kwa magonjwa sugu yasiyoambukiza kama saratani, figo, moyo, sukari, mifupa na mishipa ya fahamu.
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa uamuzi huo ni sehemu ya dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kulinda afya za Watanzania, kuimarisha mfumo wa huduma za afya na kuhakikisha hakuna mwananchi atakayeshindwa kupata matibabu muhimu kutokana na ukosefu wa uwezo wa kifedha.
Ameyasema hayo leo Ijumaa, Februari 6, 2026 wakati wa kuahirisha Mkutano wa Pili wa Bunge la 13 jijini Dodoma, ambapo amesisitiza kuwa Serikali imepata mafanikio makubwa katika sekta ya afya ikiwemo kuongeza wigo wa upatikanaji na ufanisi wa utoaji wa huduma za afya nchini.
“Sote tunakumbuka kuwa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania alitoa ahadi mbalimbali kwa wananchi. Ahadi hizo ni pamoja na zile zitakazotekelezwa ndani ya siku 100 baada ya Serikali kuingia madarakani.”
Waziri Mkuu ametaja mafanikio mengine yaliyopatikana katika sekta ya afya ni pamoja na kuendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote kwa awamu ya majaribio ambao unahusisha makundi maalum ya watoto, wajawazito na wenye ulemavu.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali imeondoa zuio la kuchukua miili ya marehemu katika vituo vya umma vya kutolea huduma za afya kwa kigezo cha madeni ya matibabu, imeajiri watumishi wa afya 5,000 na kuwapangia vituo vya kazi kote nchini na imefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya afya.
”Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 39 ili kuboresha huduma za uzazi na watoto wachanga katika vituo 89 vya kutolea huduma za afya na imeongeza vituo vya upasuaji wa dharura kutoka vituo 523 Oktoba, 2025 hadi vituo 578 Januari, 2026.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali imeongeza uwezo wa Taifa kukabiliana na athari za VVU na UKIMWI kwa kuhakikisha utoshelevu wa dawa za kufubaza makali ya UKIMWI kwa kufufua Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries (TPI) kilichopo mkoani Arusha na kuongeza fedha za ndani kupitia Mfuko wa Udhamini wa Afua za UKIMWI.








0 comments:
Post a Comment