WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Februari 6, 2026 ameahirisha Mkutano wa Pili wa Bunge la 13 jijini Dodoma na kutumia fursa hiyo kuwaasa Watanzania wote kuwa na matumizi chanya ya mitandao ya kijamii na kuifanya kuwa nyenzo muhimu ya kujielimisha, kuendeleza biashara na kueneza ujumbe wa mshikamano.
Pia, Mheshimiwa Dkt. Nchemba ameiagiza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum iweke kipaumbele cha kutoa elimu ya malezi bora katika kijamii kwa kushirikiana wadau mbalimbali wakiwemo Viongozi wa Asasi za Kiraia na Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Waziri Mkuu amesema suala la amani, usalama na utulivu ni jukumu la kila Mtanzania na linahitaji juhudi za pamoja katika nyanja mbalimbali, hivyo wote wanawajibika kuepuka masuala yote yanayochochea uvunjifu wa amani ikiwemo matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
Aidha, Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa rai kwa Watanzania wote kuendelea kulinda Tunu za Taifa kwa kuwa ni wajibu wa kila raia kuziheshimu na kuziendeleza ili kuleta mshikamano na kuimarisha heshima ya Taifa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuwawezesha wananchi kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya biashara ndogo za kati na kampuni changa.
“Tarehe 05 Februari, 2026 nilishiriki kwenye tukio muhimu la uzinduzi wa utoaji mitaji yenye thamani ya shilingi bilioni 200 ili kuwawezesha wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara, maafisa usafirishaji, wasanii na kampuni changa za vijana kuongeza mitaji, kukuza biashara na kuchangia ajira na ukuaji wa uchumi.”
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutoa mikopo mingine yenye masharti nafuu kupitia mifuko mbalimbali na kunufaisha wafanyabiashara wadogo, wajasiriamali na kampuni changa kwa kuwatambua na kuwasajili wafanyabiashara wadogo zaidi ya milioni moja na kuwapatia mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 707.4 kutoka taasisi za fedha za NMB, DCB na TCB.
Vilevile, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametoa rai kwa Watanzania kuendelea kutumia taasisi za kifedha zilizo rasmi na kuepuka taasisi zisizokuwa na usajili . “Hakuna benki yenye masharti mabaya kuliko yale ambayo baadhi ya Watanzania wanayapata kwenye kausha damu. Tusiziogope taasisi rasmi ili kujiepusha na matatizo ambayo yamekuwa yakijitokeza kwenye baadhi ya taasisi ambazo hazijasajiliwa.”









0 comments:
Post a Comment