Nafasi Ya Matangazo

February 27, 2026




🔴Ni baada ya kueleza kero yake kwa Waziri Mkuu

JITIHADA za Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba kusikiliza kero za wananchi zimezaa matunda ambapo mkazi wa Kata ya Baraa jijini Arusha, Bi. Agnes Simon Laizer alilipwa fidia ya sh. milioni 7 na mmiliki wa shule ya Nariva Hill (jirani yake) ambaye alikuwa ameharibu jiko na ukuta kutokana na ujenzi wa ghorofa unaoendelea.

Bi. Agnes alikabidhiwa fedha hizo taslimu jana (Alhamisi, Februari 26, 2026) mbele ya mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa, Bw. Polycarp Nkuyumba, Diwani wa Kata hiyo, Mtendaji wa Kata na Mtaa, pamoja na Maafisa wa Wilaya waliokuwa wameambatana na timu ya Wasaidizi wa Waziri Mkuu waliokuwa wakisikiliza kero za wananchi kama alivyoelekeza Waziri Mkuu.

Februari 24, mwaka huu, Bi. Agnes Laizer aliwasilisha kero yake mbele ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo linapojengwa soko jipya la Kilombero wakati akiwa kwenye ziara ya siku tatu mkoani Arusha. Bi. Agnes alisema ameathirika kiafya kutokana na ujenzi wa ghorofa kwenye shule ya msingi ya Nariva ikiwemo kuharibiwa ukuta na kubomolewa jiko lake.

Alisema vumbi, zege, vipande vya matofali na mbao vinafika katika eneo lake (kwa kuwa hajaweka neti ya kuzuia), sehemu ya ghorofa imezidi katika eneo lake na bomba lake la maji ya kunywa lililochimbuliwa wakati ujenzi ukianza, bado halijafukiwa.

Februari 25, 2026 Bi. Agnes alifika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambako timu ya wataalamu wa Mkoa na Jiji walikutana na kusikiliza kero za wananchi na wakaamua kumuita mmiliki wa shule ya Nariva Hill, Bw. Emmanuel Saanya ambaye alikubali kulipa fidia kwa mama huyo.

Timu iliyofika nyumbani kwa Bi. Agnes Laizer ilishuhudia ujenzi wa ghorofa ukiendelea bila kuwepo kwa nyavu za kuzuia hatari (safety nets), mabomba ya maji yaliyokatika na jiko lililokuwa limebomoka, likiwa limeshakarabatiwa.

Akitoa shukrani baada ya kukabidhiwa fedha hizo, Bi. Agnes alisema anashukuru kwa kulipwa fidia hiyo ambayo ataitumia kukarabati nyumba yake. Alimshukuru Rais Dkt.  Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mawakili wanaotoa msaada wa kisheria ambao kwa sehemu kubwa walishiriki kutatua mgogoro huo.
Posted by MROKI On Friday, February 27, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo