Mkuu wa wilaya ya Arusha, Joseph Mkude akikabidhi sh. milioni 1.8 kwa Flora Mbeve aliyeomba msaada kwa Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba wa kulipiwa deni la kikoba.
Mwenyekiti wa kikundincha Jikomboe, Laurent Mwita Marwa akisaini mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha kukiri kupokea rejesho la sh. milioni 1.8 kutoka kwa Bi. Flora Mbeve.🔴Akabidhiwa sh. milioni 1.8 kulipa deni la kikoba
MKAZI wa Arusha, Bi. Florah Mbeve amekabidhiwa sh. milioni 1.8 ili akalipe deni analodaiwa kwenye kikoba ambazo alikopa na kumpa mumewe kisha akatelekezwa na mwanaume huyo kwa madai kuwa anazaa watoto wa kike tu.
Februari 24, mwaka huu, Bi. Florah aliwasilisha kero yake mbele ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo linapojengwa soko jipya la Kilombero wakati akiwa kwenye ziara ya siku tatu mkoani Arusha. Alisema alikuwa anauza vipande vya matikiti ili apate fedha za kujikimu na wanawe wanne na kiasi apeleke kwenye rejesho.
Bi. Florah alikabidhiwa fedha hizo taslimu jana (Alhamisi, Februari 26, 2026) na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude kwa niaba ya Waziri Mkuu ambaye aliahidi kumsaidia mama huyo.
Akimkabidhi fedha hizo ofisini kwake mbele ya Mwenyekiti wa kikundi cha Jikomboe, Bw. Laurent Mwita Marwa, Mkuu huyo wa Wilaya ya Arusha alisema kuwa amemkabidhi kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Waziri Mkuu kama ambavyo aliahidi kwamba atampatia fedha hiyo ili kumuondolea adha na usumbufu alioupata kutokana na deni hilo analodaiwa kwenye kikoba.
Akizungumza baada ya kupokea fedha hizo, Bw. Marwa alishukuru kupewa rejesho la mama huyo kwa mkupuo kwa sababu tangu mama huyo alipojifungua, alikuwa hana chanzo cha uhakika cha fedha cha kuweza kurejesha mkopo wake.
Akitoa shukrani baada ya kukabidhiwa fedha hizo, Bi. Florah alisema amefurahi sana na akamshukuru Waziri Mkuu kwa msaada huo wa fedha alioupata kwa kuwa fedha hiyo amekuwa akidaiwa kwa muda mrefu na akashindwa kurejesha baada ya mumewe kumtelekeza yeye na watoto wake.
“Ninamshukuru sana Waziri Mkuu, ninamshukuru Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutujali wananchi wake. Fedha nilizopewa zimenisaidia kulipa deni kwenye kikoba, deni ambalo mume wangu aliniachia na kunitelekeza na watoto, kwa sasa nina amani, nina tumaini la kuishi,” alisema Bi. Florah.









0 comments:
Post a Comment