Nafasi Ya Matangazo

February 27, 2026






🔴DC atoa siku tatu watoto wa bweni warejeshwe makwao

ZIARA ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba jijini Arusha imewazindua watendaji na kujikuta wakibaini ujenzi wa shule ya ghorofa usio na vibali na watoto kulazwa katika bweni wakati ujenzi ukiendelea kwenye ghorofa hizo.

Hayo yamebainika leo (Ijumaa, Februari 27, 2026) wakati Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude na Kamati ya Usalama ya Wilaya walipofanya ziara kwenye shule ya Nariva Hill na kufanya ukaguzi katika madarasa, mabweni, jikoni na eneo wanalojenga ghorofa juu ya bweni lililokuwa linatumika.

Katika ziara hiyo shuleni hapo ambayo ilikuwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu, viongozi hao walibaini kuwepo kwa msongamano wa wanafunzi wa kike wanaolala katika bweni la muda ilhali hawana vyoo wala mabafu kwenye ghorofa yao. Pia walibaini baadhi ya watoto wanalala wawiliwawili kwenye kitanda kimoja.

“Yale mabweni sikuona standards za Wizara ya Elimu, kuanzia leo natoa muda wa siku tatu tu kwa sababu hawa watoto wana kwao; kwa hiyo wazazi wao lazima wajulishwe. Natoa siku tatu mabweni haya yawe yamefungwa. Tumepewa tahadhari ya magonjwa ya kipindupindu na mfumo wa hewa, hali iliyopo mabwenini haipo sawa, yafungwe warudi kusoma shule ya kutwa,” amesema Mkuu huyo wa Wilaya.

Pia amesitisha ujenzi unaoendelea shuleni hapo kwa kuwa hawana vibali vya ujenzi licha ya kuwa walishapewa stop order tangu Oktoba 13, 2025 lakini wakakaidi na kuendelea na ujenzi. “Stop order ilitolewa tangu mwezi wa Oktoba na haikuzingatiwa. Kwa hiyo, kuanzia leo, ianze kutekelezwa hadi vibali kamili vitakapotolewa,” amesema.

Vilevile amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha na Mkaguzi wa Elimu wafuatilie barua halisi zilizoruhusu usajili wa shule hiyo ikiwemo nakala za vibali vya kuruhusu kulaza watoto shuleni.

 “Walete nakala za vibali kutoka wizara ya elimu na haraka viwasilishwe kwenye ofisi ya TAKUKURU ya Wilaya ili wafanye uchunguzi zaidi,” amesisitiza.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema hali ya jikoni shuleni hapo ni chafu, hakuna bwalo na watoto waliopo shuleni ni zaidi 1,700. Amewataka wamiliki wa shule hiyo wazingatie viwango vya wizara ya elimu vya ujenzi wa jiko.

Kuhusu maji yanayotumiwa na wanafunzi, Mkude amesema eneo la maji ya kunywa ni finyu na watoto wanapokezana vikombe vya kunywea maji kutoka kwenye tenki. 

Amewataka waweke mifumo ya mabomba kama ilivyoelekezwa na wizara ya elimu ambapo mabomba mengi huwekwa kwa pamoja na watoto wanaweza kunywa bila kupanga foleni.

Mapema, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Javelin Gaspar alisema shule hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2016, ina wanafunzi 1,726 wanaosoma kuanzia shule ya awali hadi darasa la saba. “Shule ina madarasa 55, walimu 42, mabweni mawili ambapo wanafunzi wanaolala shuleni ni 162.

Alipoulizwa kuhusu uwepo wa vibali vya ujenzi, mmiliki wa shule hiyo, Emmanuel Saanya na mshauri wa ujenzi wa shule hiyo, Emmanuel Rajab walikiri kutokuwa na vibali vya ujenzi.

Mkuu wa Wilaya hiyo alimwagiza Kamanda wa Polisi wa Wilaya, Georgina Matagi aende nao polisi wakatoe maelezo yao leo hii hii. 
Posted by MROKI On Friday, February 27, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo