Ikiwa ni takribani miaka 30 imepita tangu ianzishwe Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Julai 1, 1996, Mamlaka hiyo inajivunia maendeleo, uwazi, mageuzi na mabadiliko chanya ya kimifumo yaliyofanyika ambayo yamekuwa chachu ya kufikia malengo ya Mamlaka hiyo na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Akizungumza kuhusiana na mafanikio hayo, Juni 28, 2026, Jijini Dodoma, Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Paul Walalaze, anasema imekuwa ni miaka 30 ya mafanikio mengi na Mamlaka inajivunia utendajikazi na ushirikiano mkubwa wanaoupata kutoka kwa walipakodi na wananchi katika ujenzi wa taifa.
"Kama ambavyo TRA inawajibika kukusanya kodi, katika miaka hii 30, tumeweza kuongeza makusanyo kutoka shilingi bilioni 531 kwa mwaka wa fedha 1996/1997 hadi trilioni 32 mwaka 2025/2026, ongezeko hili ni kubwa na ndiyo maana serikali inafanya mambo makubwa ya kimaendeleo kwa wananchi wake, kwani fedha za kufanya hayo zipo," amesema Walalaze.
Aidha, Walalaze anasema, TRA imefanikiwa kuwafikia wanafunzi, walipakodi na wananchi wengi kuwapa elimu ya kodi.
"TRA tunakwenda walipo wadau wetu, yaani shuleni, vyuoni, sehemu za kazi, viwandani na kwenye biashara ili kuwapa elimu. Pia tunashirikiana na taasisi za elimu kufundisha masuala ya kodi, kutumia vipeperushi, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, hii yote ni kuhakikisha kila raia anakuwa na uelewa wa masuala ya kodi na ashiriki katika kulipa kodi," amesema.
Sambamba na hilo, Meneja huyo wa Elimu ya Mlipakodi, anasisitiza kuwa, Mamlaka ya Mapato imeimarisha matumizi ya teknolojia katika utendaji na usimamizi wa kodi ili kufikia malengo yaliyowekwa.
"Kwa kiwango kikubwa sana, Mamlaka imehama kutoka kwenye matumizi ya karatasi na sasa tupo kidijitali zaidi. Mathalani, usajili wa walipakodi, malipo ya kodi, utoaji wa risiti, masuala ya forodha na mengine mengi yanafanyika kwa njia ya mtandao."
"Tulipoanza kutumia teknolojia, baadhi walikuwa na hofu, lakini leo, walipakodi wenyewe wanafurahia kwani hawana ulazima wa kufikia katika ofisi za TRA kuhudumiwa, wanafanya shughuli zao kule kule walipo, na Mamlaka inapata taarifa zao," amesema.
Katika hatua nyingine, Walalaze anasema, katika miaka 30, Mamlaka inajivunia kuongezeka uwazi na uwajibikaji ambao umekuwa nyenzo muhimu ya kufikia malengo na maendeleo.
"Sasa hivi hakuna janjajanja, utendajikazi na shughuli za kikodi zinafanyika kwa uwazi, na uwazi huu umeongeza uwajibikaji na uadilifu kwa watendaji wa Mamlaka na walipakodi pia," amesisitiza.
Vilevile, Mamlaka imefanikiwa kujenga uhusiano mzuri kati yake na walipakodi. Anasisitiza kuwa, kumekuwa na mafanikio ya kujenga uhusiano mzuri ambao umekuwa chachu ya ongezeko la makusanyo ya kodi, kwani meza ya mazungumzo ipo na inatumika vyema kufikia muafaka wa ulipaji kodi.
"Eneo la uhusiano mzuri limefanikiwa sana hasa kufuatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais wetu, Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye anasisitiza majadiliano yachukue nafasi na kuachana na matumizi ya mabavu katika ukusanyaji wa kodi, na hapa niseme tumefanikiwa sana, na tija yake imeakisi katika ongezeko la mapato," amesema Walalaze.
Mafanikio mengine, ni kuimarika kwa mazingira ya biashara na uwekezaji. Walalaze anasisitiza kuwa wafanyabiashara na wawekezaji ni mashahidi wa namna Mamlaka ilivyoweka mazingira mazuri ya ufanyikaji wa shughuli za biashara na uwekezaji, na hili limesaidia kuongezeka kwa idadi ya wafanyabiashara ambao ni chachu ya kukuza uchumi na maendeleo nchini.
Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, TRA inapaswa kukusanya shilingi trilioni 36.99 ili kufanikisha bajeti nzima ya serikali ya shilingi trilioni 62.33, hivyo TRA inahimiza walipakodi na wananchi kwa ujumla kutimiza wajibu wa kulipa kodi kwa hiari ili kufikia malengo ya serikali ya kukuza uchumi na kuboresha ustawi wa wananchi.
Ikumbukwe kuwa, Julai 1, 2026, Rais Dk. Samia atatoa tuzo kwa walipakodi mahiri kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa walipakodi katika ujenzi wa taifa na kujenga motisha kwa walipakodi kuendelea kulipa kodi.
Sambamba na hilo, Walalaze ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi, Julai 2, katika uwanja wa KMC Complex, ambapo kutakuwa na mechi ya kirafiki kati ya timu ya TRA United na URA FC kutoka Uganda, ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya miaka 30 ya mafanikio kwa kuzingatia TRA inashirikiana na mamlaka nyingine za ukusanyaji kodi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Katika mechi hiyo, hakuna kiingilio, yaani ni bure.







0 comments:
Post a Comment