Wanafunzi
wa shule ya Fountain Gate Academy wakisikiliza wakati wa hafla fupi ya kusaini hati
ya makubaliano ya kuanzisha na kusimamia programu ya uchunguzi wa magonjwa ya
moyo kwa wanamichezo wa Academy hiyo iliyofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) jana jijini Dar es Salaam.

Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya (JKCI) Dkt. Angela Muhozya na
Mkurugenzi wa Fountain Gate Sports Academy Japhet Makau wakibadilishana hati ya
makubaliano ya kuanzisha na kusimamia programu ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo
kwa wanamichezo wa Academy hiyo jana wakati wa hafla fupi ya kusaini hati hiyo
Jijini Dar es Salaam.
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya (JKCI) Dkt. Angela Muhozya na
Rais wa Fountain Gate Sports Academy Japhet Makau wakionesha hati ya
makubaliano ya kuanzisha na kusimamia programu ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo
kwa wanamichezo wa Academy hiyo wakati wa hafla fupi ya kusaini hati hiyo
iliyofanyika jana Jijini Dar es Salaam. Picha
na Jeremiah Ombelo
****************
Na Shose Romwald - Dar es
salaam.
16/06/2025 Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Klabu ya Fountain Gate Academy na
Chama cha Madaktari wa Michezo Tanzania (TMSA) wasaini makubaliano kuanzisha na
kusimamia programu ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa wanamichezo wa academy
hiyo.
Akizungumza wakati wa kusaini
makubaliano hayo jana jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema makubaliano hayo
yamelenga kufanya uchunguzi wa awali wa moyo kwa wachezaji wa Fountain Gate FC
pamoja na wanafunzi wa shule 15 zinazomilikiwa na Academy hiyo.
“Makubaliano haya yatatoa
fursa kwa wanafunzi wa Fountain Gate waliopo katika shule 15 zilizopo mikoa
mbalimbali ya Tanzania wanaoshiriki katika shughuli za michezo mbalimbali
ikiwemo mpira wa miguu”, alisema Dkt. Angela
Dkt. Angela alisema mpango huo
wa kuanzisha sports cardiology program inayohusisha pre-participation cardiac
screening kwa wanamichezo ni hatua muhimu katika kuhakikisha usalama wa
wanamichezo nchini.
“Lengo letu ni kubaini mapema
matatizo ya moyo ambayo yanaweza kuwa hatari na yasiyoonekana kwa macho ili
kuyazuia kabla hayajasababisha madhara makubwa”,
“Hii ni pamoja na kuzuia vifo
vya ghafla vya moyo (sudden cardiac death), ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa
duniani kote kwa wanamichezo, hata wale waliokuwa wakionekana kuwa na afya
njema”, alisema Dkt. Angela
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Fountain Gate Academy Japhet Makau alisema Taasisi hiyo imepata fursa ya kushirikiana
na JKCI kulinda afya za wachezaji wake na kuwaweka watoto katika mikono salama kwa
kuwafanyia vipimo vya moyo kabla ya kuingia kwenye michezo.
Makau alisema Taasisi yake
inaamini JKCI itaondoa hofu kwa wachezaji wakati wapo uwanjani na kuwajenga
vijana kujiamini hivyo kuongeza nguvu katika michezo yao.
Progamu hiyo mpya na ya
kipekee ni sehemu ya upanuzi wa huduma za kinga inayofanya na JKCI katika
jamii, na kuelekeza nguvu katika kuzuia vifo vya ghafla vya wanamichezo hasa
kwa vijana wanaoshiriki michezo.
Programu hiyo imesainiwa mara
baada ya JKCI kusaini mkataba na Shirika la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) hivi
karibuni wakiwa na lengo la kuwalinda wachezaji na madhara yanayoweza
kujitokeza pindi wanapokuwa uwanjani.
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya (JKCI) Dkt. Angela Muhozya na
Rais wa Fountain Gate Sports Academy Japhet Makau wakiwa katika picha ya pamoja
na wanafunzi wa Fountain Gate Academy mara baada ya kusaini hati ya makubaliano
ya kuanzisha na kusimamia programu ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa
wanamichezo wa Academy hiyo iliofanyika jana Jijini Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment