Mradi
wa Kuimarisha Ustahimilivu wa Bioanuwai ya Misitu ya Mazingira Asilia dhidi ya
Matishio ya Mabadiliko ya Tabianchi, unaotekelezwa na Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP), umeendelea kuimarisha miundombinu ya uhifadhi katika Hifadhi ya
Pindiro, wilayani Kilwa.
Katika
ziara ya ukaguzi iliyofanywa na Kamati ya Utekelezaji ya mradi huo, maendeleo
ya ujenzi wa majengo muhimu ya hifadhi hiyo yalionekana kufikia asilimia 46.
Ujenzi huo unahusisha jengo la utalii, vyoo, jengo la walinzi na geti la
kuingilia, kwa gharama ya Sh milioni 297. Mkandarasi anayetekeleza kazi hiyo ni
kampuni ya Strider Engineering Ltd, huku mradi ukitarajiwa kukamilika Oktoba
2025.
Akizungumza
wakati wa ukaguzi huo, Mhandisi Hendry Sanga kutoka kampuni ya Strider
Engineering alisema kuwa kazi inaendelea vizuri na kwamba wanazingatia viwango
vya ubora pamoja na muda wa utekelezaji kama ilivyokubaliwa.
“Tunaendelea
na kazi kwa kasi nzuri, tukizingatia viwango vilivyokubaliwa. Lengo ni
kuhakikisha tunakamilisha mradi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa,” alisema
Sanga.
Naye
Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi kutoka TFS, Bw. Fridolin Matembo, alieleza
kuridhishwa na mwenendo wa utekelezaji wa mradi huo.
“Mkandarasi
anafanya kazi nzuri. Kasi ya utekelezaji ni ya kuridhisha, lakini tunasisitiza
umuhimu wa kukamilika kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu,” alisema Matembo.
Katika
hatua nyingine, hifadhi ya Pindiro imekabidhiwa pikipiki mbili mpya kwa ajili
ya kusaidia kazi za uhifadhi. Vifaa hivyo ni sehemu ya mchango wa UNDP
ulioainishwa wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi huo katika Hifadhi ya
Kazimzumbwi, mkoani Pwani.
Akikabidhi
vifaa hivyo, Mratibu wa Mradi, Bw. Mteleka Someni Lusugu alisema:
“Pikipiki
hizi ni sehemu ya vifaa muhimu tulivyopokea kupitia UNDP. Zitatumika kuongeza
ufanisi katika shughuli za uhifadhi, hasa maeneo yenye changamoto za
miundombinu ya usafiri,” alisema Lusugu.
Mradi
wa Bioanuwai unatekelezwa kwa kipindi cha miaka sita katika maeneo mbalimbali
ya misitu ya asili nchini. Lengo kuu ni kuimarisha usimamizi wa rasilimali
misitu, kuongeza ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari za mabadiliko ya
tabianchi, pamoja na kuboresha miundombinu na huduma za uhifadhi kwa maendeleo
endelevu ya wananchi na taifa kwa ujumla.



0 comments:
Post a Comment