SERIKALI imesema wananchi walioandikishwa katika daftari la kudumu la wapigakura mwaka 2015 na mwaka 2019/2020, kadi zao ni halali kwa mujibu wa kifungu cha 168 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Namba 1 ya mwaka 2024.
Pia, imesisitiza kadi hizo zitatumika katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani mwakani. Msisitizo huo wa serikali, umetolewa kufuatia baadhi ya wananchi kufi ka katika vituo vya uboreshaji daftari la wagipakura, katika mikoa, inayoendelea na utaratibu huo, kwa lengo la kubadilisha kadi za kupigia kura.
Kauli hiyo, ilitolewa bungeni jijini hapa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipoahirisha mkutano wa 16 wa Bunge. Majaliwa, alisema hadi hivi sasa, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imekamilisha uboreshaji wa daftari hilo katika Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Kagera, Geita, Mwanza na Shinyanga.
Alisema kuanzia Septemba 4 hadi 10, mwaka huu, uboreshaji wa daftari, utaendelea katika mikoa ya Mara, Simiyu na sehemu ya Mkoa wa Manyara katika Halmashauri za Wilaya za Babati, Hanang’, Mbulu na Babati Mji.
Kwa mujibu wa kifungu cha 9(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Namba 1 ya mwaka 2024, uboreshaji wa daftari hilo, unahusisha Watanzania wenye sifa za kuandikishwa kuanzia umri wa miaka 18 au zaidi.
Alizitaja sifa nyingine ni wale watakaotimiza umri huo wakati wa uchaguzi mkuu mwakani.
“Uboreshaji wa daftari, unatoa fursa kwa wapigakura walioandikishwa kwa bahati mbaya kadi zao zimepotea au kuharibika, wale aliohama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda lingine au kuhamisha taarifa zao kufika vituoni kupata kadi mpya.
“Zoezi hili, halihusishi kubadilisha kadi za wapigakura zenye jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kupata kadi iliyoandikwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
“Kwa kuzingatia maboresho hayo, niwatoe wasiwasi wananchi wote walioandikishwa mwaka 2015 na mwaka 2019/2020 kwamba, kadi zao ni halali kwa mujibu wa kifungu cha 168 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Namba 1 ya mwaka 2024, zitatumika katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani wa Mwaka 2025,”alisema.
UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA
Waziri mkuu, alisema Tanzania, imekuwa na utaratibu wa kujenga misingi ya uongozi kuanzia ngazi za chini, kuiwezesha serikali kuwafi kia watu wake katika kuleta maendeleo endelevu.
Alisema mwaka huu, kutakuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji ambao unatarajiwa kufanyika Jumatano ya Novemba 27, mwaka huu.
“Kazi za msingi zilizokamilika mpaka hivi sasa ni kuandaliwa kanuni za uchaguzi wa viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa katika Mamlaka za Wilaya na Miji, Mwongozo wa Elimu ya Mpigakura na Mwongozo wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” alieleza.
Alitaja maandalizi mengine yanajumuisha kutangaza orodha ya maeneo ya utawala, uhakiki wa vituo vya kupigia kura awamu ya pili na manunuzi ya vifaa vya uchaguzi.
“Hivi sasa, mamlaka husika zinaendelea na utoaji wa elimu ya mpiga kura kupitia vyombo vya habari, mabango na mitandao ya kijamii,” alisema.
Source: Gazeti la Uhuru.
0 comments:
Post a Comment