Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza na wadau mbalimbali waliojitokeza kwenye Mdahalo wa Kitaifa wa Kumbukumbu ya Miaka 40 ya kifo cha Hayati Edward Moringe Sokoine uliofanyika leo tarehe 8 Aprili, 2024 katika Ukumbi wa Multipurpose Chuo cha Kilimo SUA, Morogoro (Picha na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu)
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, Watanzania wanapaswa kumuenzi Hayati Edward Moringe Sokoine kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuinua uchumi wa nchi na kuboresha maisha yao.
Dkt. Biteko amesema hayo leo
wakati akimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Mhe. Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi kufungua Mdahalo wa Kitaifa wa Kumbukizi ya
Miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine iliyofanyika Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo (SUA), mkoani Morogoro.
Dkt. Biteko amesema Hayati
Sokoine atakumbukwa daima kama kiongozi aliyepigania maendeleo ya taifa kwa
moyo wake wote na katika uongozi wake katika nyadhifa zote alitilia mkazo
wananchi kuwa ndio msingi wa maendeleo.
"Hayati Sokoine alifanya
kazi kubwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya taifa na aliweka misingi
imara iliyoendeleza muongozo wa kila kiongozi wa Tanzania awe wa namna
gani," amesema Dkt. Biteko
Amesema, Hayati Sokoine
aliwataka Viongozi wa Serikali na wananchi kueleza wamezipata mali kwa namna
gani kwa hiyo watu wengi waliopata mali kwa njia haramu walimuogopa Sokoine
walitupa fedha na mali nyingine kwa kuhofia kuhojiwa.
Vile vile, Dkt. Biteko
amesisitiza Sekta ya Kilimo iwe kimbilio katika kuinua na kuboresha maisha ya
wananchi.
Amesema sekta hiyo ina mchango
mkubwa katika kuleta maendeleo kwa kuwa imeajiri watanzania wengi hususan
vijana na kukipongeza chuo cha SUA kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya
Sekta ya Kilimo nchini.
Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi
na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema Hayati Sokoine amefanya kazi kubwa
katika maendeleo ya Sekta ya Kilimo na kuongeza kuwa Wizara ya elimu inafanya
kazi kubwa kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na na mchango mkubwa kwa wananchi
hususan vijana.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu
wa Chuo cha SUA, Prof. Raphael Chibunda amesema kuwa, Edward Moringe Sokoine
alikuwa kiongozi wa kipekee hasa katika suala la kutoa maamuzi, uzalendo,
uchapa kazi, uadilifu na uaminifu.
"Kwa mfano, alifanya kazi
bila kuchoka usiku na mchana, pia alisimamia sera za nchi kwa bidii na kwa
weledi. Alichukia na alipiga vita ruswa na kuhakikisha nchi inapiga hatua
katika maendeleo kiuchumi na kijamii," amesema Prof. Chibunda.
Mdahalo wa kumbukizi ya miaka
40 ya kifo cha Sokoine umejadili mambo yanayohusu uongozi na mambo ambayo taifa
la Tanzania limerithi kutoka kwa Sokoine ikiwemo Sokoine na Uongozi
iliyowasilishwa na Mhe. Anna Makinda, Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Pia, Uongozi na Maendeleo
iliwasilishwa na Prof. Issa Shivji, Kilimo na Maendeleo iliyowasilishwa na Jaji
Mstaafu Joseph Sinde Warioba ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUA na
Sokoine na Maendeleo ya kilimo iliyowasilishwa na Prof. Kalunde Sibuga ambaye
ni nguli wa kilimo wa chuo cha SUA.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, Watanzania wanapaswa kumuenzi Hayati Edward Moringe Sokoine kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuinua uchumi wa nchi na kuboresha maisha yao.
0 comments:
Post a Comment