Mashabiki wa michezo na wakimbiaji nchini wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi kwenye The SQF Zanzibar Cleft Marathon – Season 7, mbio maalum zinazolenga kuchangisha fedha kwa ajili ya watoto waliozaliwa na tatizo la mdomo na taya wazi (cleft).
Mbio hizo zimepangwa kufanyika Desemba 21, 2025 katika viwanja vya New Aman Complex visiwani Zanzibar, na zimekuwa kivutio kikubwa kwa wanamichezo, wadau wa afya, pamoja na wananchi wanaoguswa na masuala ya kijamii.
Kwa mujibu wa waandaaji, The Same Qualities Foundation (SQF), usajili kwa ajili ya mbio za mwaka huu umeshaanza katika maeneo mbalimbali ikiwemo New Aman Complex, Michenzani Mall, Forodhani, Masomo Bookshop, pamoja na Hospitali ya Edward Michaud jijini Dar es Salaam. Ada ya usajili ni shilingi 35,000 kwa washiriki wa mbio za 21KM, 10KM na 5KM.
Tukio hili ni zaidi ya mashindano, wamesema waandaaji. “Kila hatua unayokimbia ni sehemu ya kubadilisha maisha ya mtoto mmoja—kutoa tabasamu jipya, kuondoa unyanyapaa, na kurejesha matumaini kwa familia nzima.”
Mbio hizi zimepata pia heshima ya kuhudhuriwa na Mgeni Rasmi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, hatua inayoongeza uzito na hamasa kwa washiriki.
Kwa upande wao, wadau wa michezo wamepongeza juhudi za SQF kwa kuunganisha michezo na huduma za kijamii, wakisema mbio hizi zimekuwa mfano bora wa jinsi nguvu ya umoja inaweza kubadili maisha ya watu wanaohitaji msaada.
Waandaaji wametoa wito kwa wakimbiaji, klabu za michezo, mashirika na familia kujitokeza kwa wingi kushiriki na kuchangia. Washiriki wanaweza pia kulipia kupitia M-Pesa kwa namba 5427230 (The Same Qualities Foundation).
Mbio hizi zinatarajiwa kuwa miongoni mwa matukio makubwa ya michezo ya kijamii mwaka 2025 nchini, yakileta pamoja wanamichezo, wafadhili na watu wa kada mbalimbali kwa lengo moja—kupigania tabasamu la mtoto.





0 comments:
Post a Comment