Rais Mstaafu Jakaya Dkt. Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education - GPE) akiongea na wajumbe wa Bodi ya GPE baada ya kumalizika kwa mkutano huo mjini Brussels, Ubelgiji. Pamoja naye ni Afisa Mtengaji Mkuu wa GPE, Bi Laura Frigenti
Rais Mstaafu Jakaya Dkt. Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education - GPE) akiteta jambo na Bi. Christine nHogan, Makama mwenyekiti wa GPE wakati wa mkutano wao mjini Brussels, Ubelgiji.Rais Mstaafu Jakaya Dkt. Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education - GPE) akishiriki Mkutano wa 23 wa Kimataifa wa Qatar mjini Doha
Rais Mstaafu Jakaya Dkt. Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education - GPE) akiteta jambo na Dkt Hamad bin Abdulaziz Al Kawari, Waziri wa Nchi na Naibu Waziri Mkuu wa Qatar, mjini Doha leo. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mhe Habib Awesi Mohamed.
***************
Rais Mstaafu Jakaya Dkt. Mrisho Kikwete, ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya
Elimu Duniani (Global Partnership for Education - GPE) ameendelea na jitihada
za kukuza elimu duniani.
Kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bodi ya GPE
alisimamia Mkutano wa mwisho wa Bodi hiyo wa kuhitimisha Mpango wa 4 wa Miaka 5
wa Mzunguko wa Ufadhili wa GPE (4th financing campaign 2021 - 2025) ambao
ulifanikiwa kukusanya takriban Dola za Kimarekeni bilioni 4.1 kwa ajili ya
kugharamia uboreshaji wa elimu ya awali na ya msingi kwa watoto wanaoishi
katika nchi za kipato cha chini na zinazoendelea, hususan watoto wa kike na
wale wanaojikuta kwenye mazingira magumu kama vile ya vita, ukame, mafuriko,
nk.
Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo
uliofanyika wiki hii huko Brussels, Ubelgiji ulitathmini mkakati wa kukusanya
fedha uliofanyika kwa mafanikio katika kukusanya fedha kupitia utaratibu wa
misaada (grants) na ufadhili wa pamoja (co - financing) ambapo nchi
zinazonufaika na miradi ya GPE huchangia kiasi cha fedha kwenye sekta ya elimu
na GPE huongezea kiasi kinachobakia kwa makubaliano maalumu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na GPE, kiasi
hicho cha Dola za Marekani milioni 4.7 kilichopatikana kimesaidia kuboresha
elimu kwa watoto takriban milioni 372 duniani kote huku watoto milioni 10 zaidi
wakiandikishwa shule. Aidha, kupitia ufadhili wa GPE, walimu milioni 4.7 kote
duniani walipatiwa mafunzo ya kuwaongezea ujuzi.
Aidha, Mkutano huo ulipokea taarifa ya mkakati
wa utekelezaji wa mpango mpya wa 5 wa kampeni ya ufadhili wa GPE utakaoanza mwaka 2026 hadi 2030. Kampeni hiyo imelenga
kukusanya Dola za Marekani milioni 5 na
itaongozwa kwa pamoja kati ya Rais Bola Tinubu wa Nigeria na Waziri Mkuu
Giorgia Meloni wa Italia. Fedha zitakazopatokana
kutokana na kampeni hiyo zitaongeza wigo wa GPE kuhudumia watoto takriban
milioni 750 kote duniani kwa kuwapatia elimu bora zaidi inayoendana na mahitaji
ya karne ya 21.
Vilevile, Mkutano huo ulishukuru baadhi ya
nchi ambazo zimeahidi kuendeleza
ushirikiano na GPE kama vile Ujerumani ambayo tayari imeahidi kuchangia kampeni
hii mpya ya GPE kiasi cha Dola za Marekani milioni 320 kwa kipindi cha miaka 6
ijayo.
Kwa kuzingatia mabadiliko ya sasa ya hali ya
kifedha duniani ambapo wafadhili mbalimbali, hususan nchi zilizoendelea,
zinabadilisha vipaumbele vyao vya maeneo ya kuelekeza ufadhili, Taasisi ya GPE
imelenga kuendelea kuhakikisha inasimamia na kutumia vizuri fedha zinazotolewa
na wafadhili ili kuwanufaisha watoto wengi zaidi duniani.
Vilevile, GPE imepanga kuendelea kuzishawishi nchi
ambazo siyo wafadhili waliozoeleka wa GPE (non traditional donors) kama vile
nchi za mashariki ya kati ili ziweze kuoanisha programu zao za kusaidia elimu
duniani na zile za GPE, na kuongeza fedha zaidi wanazochangia kwa GPE.
Kama sehemu ya kutekeleza mkakati huo,
Mwenyekiti huyo wa Bodi ya GPE Dkt. Kikwete
leo amepata fursa ya kushiriki Mkutano wa 23 wa Kimataifa wa Qatar ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza utayari
wa GPE kuendelea kushirikiana na Serikali ya Qatar katika jitihada zake za
kusaidia watoto wenye mahitaji mbalimbali ya kielimu kote duniani.
Aidha, katika mazungumzo yake na Viongozi
mbalimbali wa Taifa la Qatar pambezoni mwa Mkutano huo ameeleza nia ya GPE
amepongeza mchango mkubwa wa Qatar katika elimu duniani na kuihakikishia
utayari wa GPE kuendelea kushirikiana na Serikali ya Qatar na Shirika la Qatar
la Education Above All Foundation.
GPE ni Taasisi iliyoanzishwa na Kundi la Nchi
zenye Uchumi na Utajiri Mkubwa Duniani (G7) mwaka 2002 ili kuharakisha
ufikiwaji wa lengo la elimu la kuhakikisha kila mtu, bila kujali umri, jinsia
au hali ya kijamii, anapata elimu ya msingi bila malipo na kwa usawa.
Tanzania
ni moja ya nchi 90 zinazonufaika na miradi inayotekelezwa na GPE ambapo tangu
ilipojiunga mwaka 2013 imeshapokea zaidi ya misaada yenye thamani ya Dola za
Marekani milioni 344 kusaidia jitihada zinazofanywa na Serikali kuendeleza
elimu ya awali na ya msingi.








0 comments:
Post a Comment