Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Kibiti, Mhe. Twaha Ally Mpembene, aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali wa kuweka huduma za Wakala wa Forodha katika Bandari ya Nyamisati.
***********
Na: Josephine Majura, WF, Dodoma
Serikali imesema kuwa inatarajia kufungua Ofisi za Forodha
katika Bandari ya Nyamisati mkoani Pwani katika Mwaka wa Fedha 2024/25, baada
ya tathmini iliyofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuonesha kuwa
mazingira yanaruhusu uwepo wa Ofisi hiyo.
Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa
Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa
Kibiti, Mhe. Twaha Ally Mpembene, aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali wa
kuweka huduma za Wakala wa Forodha katika Bandari ya Nyamisati.
Mhe. Chande alisema kuwa uamuzi wa kuanzisha Kituo cha
Forodha eneo hilo unatokana na kukamilika kwa tathmini iliyofanywa na TRA na
kujiridhisha na mawanda ya shughuli zinazofanyika katika eneo hilo.
“Serikali itahakikisha mapema mwaka ujao wa fedha, Ofisi ya
Forodha katika Bandari ya Nyamisati iwe imekamilika na kuanza kutoa huduma”,
alisema Mhe. Chande.
Aidha Mhe. Chande aliahidi kuambatana na Mbunge wa eneo hilo
ili kusikiliza maoni ya wafanyabiashara walio tayari kutumia bandari hiyo na
pia kuangalia namna bora ya usafirishaji wa bidhaa katika bandari hiyo.
0 comments:
Post a Comment