Na John Bukuku – Dar es Salaam
Kaimu DAS wa Wilaya ya Kinondoni, Bw. Salumu Chitale, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya, ametumia Mkutano wa Umoja wa Wadau Madale Group uliofanyika Desemba 6, 2025 Jijini Dar es Salaam, kutoa wito wa mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wanachama, akisisitiza kuwa ndiyo nguzo ya mafanikio ya kikundi.
Amesema kuwa ukiwa pekee ni rahisi kushambuliwa na maadui, lakini mkiwa wamoja hakuna nguvu itakayoweza kuwatawanya, akitaja umoja kama silaha muhimu katika kufikia malengo ya pamoja.
Aidha, amebainisha kuwa wadau wanapaswa kuendelea kuwa wamoja na kushirikiana kwani maendeleo halisi hupatikana kupitia nguvu ya pamoja.
Amesema ili kuwe na ushirikiano imara, ni lazima kufuata miongozo ya kikundi, akifafanua kuwa ndio msingi unaoimarisha umoja, na kutokufuata miongozo kunasababisha kuvunjika kwa mshikamano.
Ametaja kuwa miongozo hiyo hupatikana kwa kufuata katiba ya taasisi na ili kuongoza watu ipasavyo ni lazima kuwepo uwazi. Ameongeza kuwa kila jambo linalofanywa na uongozi linapaswa kuwashirikisha wadau ili kuongeza uelewano na umoja.
Aidha, amekipongeza kikundi hicho kwa kutenga bajeti ya shilingi milioni 1.5 kwa ajili ya kununua mahitaji na kusaidia watu wenye uhitaji, kitendo alichokitaja kuwa mfano bora wa umoja na kujali jamii.
Amesema pia kuwa kupitia fedha za asilimia 10 zinazotolewa na serikali, kikundi kinatakiwa kufuata miongozo na taratibu maalum ili kustahili kupata mikopo hiyo.
Awali akizungumza, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wadau Madale Group, Issa Mnasha, ameeleza kuwa kikundi hicho kina wanachama 309 na kwa miaka 11 wamekuwa wakisaidiana kila mara mmoja wao anapopatwa na changamoto.
Aidha, amebainisha kuwa kwa mwaka 2024 na 2025 zaidi ya shilingi milioni 120 zimetolewa kusaidia wanachama waliokumbwa na matatizo mbalimbali ya misiba.
Amesema kuwa kikundi hicho kina wanachama kutoka makundi tofauti wakiwemo watumishi wa umma, na kimekuwa kikishiriki katika miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa kituo cha polisi Madale.
Aidha, amesisitiza falsafa ya kikundi akisema: “Maendeleo ya wadau, ni maendeleo ya mdau, na maendeleo ya mdau, ni maendeleo ya wadau.” 






0 comments:
Post a Comment