Nafasi Ya Matangazo

December 05, 2025









Waziri wa Nishati Mhe. Deogratius Ndejembi amezindua rasmi mita janja (smart meter) yenye lengo la kuboresha na kumrahisishia mteja kufanya manunuzi ya umeme moja kwa moja  ikiwa ni mageuzi makubwa ya teknolojia  yanayofanywa na TANESCO katika kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wateja.

Waziri wa Nishati amezindua Mita janja hizo Disemba 05, 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), na kuhudhuriwa na viongozi  mbalimbali wa Serikali, wadau wa sekta ya nishati na watendaji wa TANESCO.

Amesema Mita hizo mpya zinamwezesha mteja kupata umeme mara moja baada ya kufanya manunuzi ya token bila kutumia kifaa cha ziada cha kuingiza namba (CIU), hatua inayolenga kupunguza changamoto zilizokuwa zikijitokeza katika mfumo wa zamani.

“Leo tunajivunia hatua kubwa ya  kihistoria zilifanywa na TANESCO ikiwa ni  moja ya kampuni za umma inayofanya vizuri katika utoaji huduma kwa wateja nchini. Mita janja inaleta mapinduzi makubwa katika namna Shirika hili linavyofanya usimamizi wa ukusanyaji wa mapato,” ameeleza Mhe. Ndejembi.

Ameongeza kuwa changamoto zilizokuwa zikiwakabili wateja wakati wa kuingiza token ndiyo zimeisukuma Serikali kufanya mageuzi  ya kiteknolojia.

“Uzinduzi huu unaweka alama kubwa  kwa nchi yetu kwenye mapinduzi ya tekinolojia ,  hivyo naielekeza TANESCO kuhakikisha inasamabaza mita hizi maeneo yote yenye uhitaji mkuwa na kuhakikisha inaendana na viwango vya kimataifa sambamba na kutoa elimu za faida ya mita hizo,” alisisitiza. 


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema uzinduzi wa Mita Janja ni mwendelezo wa dhamira ya Serikali katika kuboresha huduma kwa wananchi.

“Nimefurahi kushuhudia hatua hii kubwa ya mapinduzi, ikiwa ni siku ya 33 tangu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani. Leo tunaweka historia muhimu kupitia uzinduzi wa Mita Janja kwa wateja wa TANESCO,” alisema Mhe. Salome.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amesisitiza umuhimu wa kulinda miundombinu ya umeme na kupongeza TANESCO kwa kuimarisha ushirikiano na vyombo vya ulinzi na usalama katika kudhibiti vitendo vya uharibifu.

“Hatua hii itukumbushe wajibu mkubwa tulionao kulinda miundombinu. Nawapongeza TANESCO kwa ushirikiano wao na Jeshi la Polisi katika kupambana na uhujumu dhidi ya miundombinu. Endeleeni kwa kasi hii ili huduma ya umeme ipatikane kwa uhakika,” alisema , Mhe. Chalamila.

Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felichesmi Mramba, ametoa pongezi kwa TANESCO kwa utekelezaji huu kwa wakati muafaka, akieleza kuwa teknolojia ya Mita Janja itarahisisha kwa kiwango kikubwa utambuzi wa changamoto za wateja kabla ya mteja kutoa taarifa TANESCO.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, Balozi Zuhura Bundala, alisema Bodi inaona fahari kuona mageuzi yanayoendelea katika uboreshaji wa huduma zinazotolewa na Shirika na kuwa bodi hiyo inazidi kupata moyo katika kuliongoza Shirika kutoa huduma bora zaidi kidigitali.
Posted by MROKI On Friday, December 05, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo