Nafasi Ya Matangazo

January 09, 2023

Na. Alfred S. Mgweno (TEMESA)
Kivuko cha MV. KAZI kimerejea rasmi katika eneo la Magogoni Kigamboni kwa ajili ya kutoa huduma baada ya kukamilika kwa ukarabati wake mkubwa uliogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 4.4.

Kivuko hicho kiliondolewa kwenye maji baada ya kufikia muda wake wa ukarabati mkubwa na kuanza rasmi kukarabatiwa mwezi Juni mwaka huu na mkandarasi Songoro Marine Transport Boatyard katika Yadi yake iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (5) 2020-2025, Serikali inayoongozwa na Rais Dr. Samia Suluhu Hassan ilitoa ahadi mbalimbali kwa wananchi ikiwemo kuboresha huduma za vivuko hapa nchini ili kuwapunguzia wananchi kero za usafiri wanazopata katika maeneo mbalimbali kupitia Wizara mbalimbali na kupitia Wizara ya Ujenzi, Serikali imeanza kutekeleza ahadi hizo kwa kuanza kuvifanyia ukarabati vivuko hivyo.

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) imedhamiria kutekeleza ahadi hizo kwa kuhakikisha kuwa vivuko vyote nchini vinakuwa vya uhakika na salama kwa matumizi ya wananchi kwa kuvikarabati na kununua vipya katika maeneo yote ya nchi yanayohitaji vivuko kadri uwezo wa bajeti ya serikali unavyoruhusu. Wakala unatekeleza ahadi hizo kwa kukarabati vivuko mbalimbali nchini kikiwemo kivuko cha MV. KAZI na ukarabati wa kivuko hicho unalenga dhamira ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa Wananchi.

Wakati nchi inapata Uhuru mwaka 1961, hapakuwa na kivuko kilichokuwa kinaendeshwa kwa injini. Vivuko vichache vilikuwa ni vya kuvutwa kwa kamba  katika baadhi ya maeneo kama Utete (Mto Rufiji), Kigongoni (Mto Ruvu), Kisauke (Mto Wami), Kirumi (Mto Kirumi) na Ruhuhu (Mto Ruhuhu) na tangu Tanzania ipate Uhuru,Serikali imenunua vivuko vipya vipatavyo ishirini na tisa (29) hadi kufikia sasa.

Kati ya vivuko hivyo, vivuko sita (6) vilipelekwa kwenye maeneo mapya ambayo hayakuwa na usafiri wa uhakika kama Chato (M.V. Chato), Kome (M.V. Kome), Ukara (MV. Nyerere), Kyanyabasa (M.V.  Kyanyabasa),  Kilambo na Msangamkuu.

Kivuko cha MV.KAZI kimekarabatiwa na kurejeshwa kwenye viwango vinavyotakiwa Kimataifa (IMO Standards) kwa kuzingatia Sheria ya Usalama wa vyombo vya majini (Shipping Merchant Act) inayosimamiwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ambalo limefanya ukaguzi na kuthibitisha kuwa kivuko ni salama kwa ubebaji wa abiria, magari na mizigo.
 
Kukamilika kwa ukarabati wa kivuko cha MV.KAZI kutaboresha huduma za mawasiliano na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali na hivyo kuongeza kasi ya maendeleo na ukuaji kiuchumi kwa wananchi wa maeneo ya Kigamboni.
 
Katika mwaka wa fedha 2022/23 Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi) kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) inatekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa vivuko na miundombinu yake ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025.

Ukarabati wa kivuko cha MV.KAZI umehusisha kufunga ijnini mpya nne, matengenezo makubwa ya (Propulsion Units), ukarabati wa milango ya kivuko, kubadilisha mabati ya kivuko yaliyochakaa na kuweka mapya, kupiga rangi umbo la kivuko, kuweka mabomba mapya ya maji na mafuta, kufunga taa mpya za kisasa, kufunga vipaza sauti, kufunga Televisheni mpya pamoja na kufunga vifaa vipya vya kisasa vya kuongozea kivuko na vifaa vya tahadhari na uokozi kulingana na viwango vinavyotakiwa Kimataifa (IMO Standards).

Kukamilika kwa ukarabati wa kivuko cha MV. KAZI kutatoa nafasi kwa kivuko cha MV. MAGOGONI kwenda kwenye ukarabati mkubwa ambao utafanywa na mkandarasi baada ya kusaini mkataba baina yake na TEMESA.

Wakala wa Ufundi na Umeme unaishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kuiwezesha kifedha kutekeleza mradi huo na kuahidi kufanya kazi kwa weledi na jitihada kubwa ili kufikia malengo na matarajio ya Serikali na wanachi kwa ujumla.

Kivuko cha MV. KAZI kina uwezo wa kubeba abiria 800 na magari 22 sawa na tani 170. 
Posted by MROKI On Monday, January 09, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo