Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizindua kitabu cha Historia ya Maisha ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa akishuhudiwa na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein na Marais wastaafu Alhaj Ally Hassan Mwinyi, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na Balozi wa Finland nchini Tanzania Mhe. Antila Sinikka katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Jumanne Novemba 12, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli baada ya kuzindua kitabu cha Historia ya Maisha ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa akiwa na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein na Marais wastaafu Alhaj Ally Hassan Mwinyi, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Jumanne Novemba 12, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza kunyanyua glasi na kumtakia maisha marefu Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa katika kuadhimisha siku ya
kuzaliwa kwake wakati wa sherehe za uzinduzi wa kitabu cha historia ya Maisha ya Mhe. Mkapa. Wengine hapo meza kuu ni Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein na Marais wastaafu Alhaj Ally Hassan Mwinyi, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na Mama Anna Mkapa katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Jumanne Novemba 12, 2019
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William na Mkewe Mama Anna Mkapa wakikata keki ya uadhimisha siku ya kuzaliwa kwake aliyoandaliwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli wakati wa uzinduzi wa
Kitabu cha Historia ya Maisha yake katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Jumanne Novemba 12, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika picha ya pamoja na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa baada ya uzinduzi wa Kitabu cha Historia ya Mhe. Mkapa. Wengine ni Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein na Marais wastaafu Alhaj Ally Hassan Mwinyi, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Balozi wa Finland nchini Mhe. Antila Sinikka na Mama Anna Mkapa na familia ya Mhe. Mkapa katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Jumanne ovemba 12, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika picha ya pamoja na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa baada ya uzinduzi wa Kitabu cha Historia ya Mhe. Mkapa wakiwa na Marais wastaafu Alhaj Ally Hassan Mwinyi na Dkt Jakaya Mrisho Kikwete katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Jumanne Novemba 12, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akijiandaa kununua Kitabu cha Historia ya Maisha ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa kutoka kwa Bi.Lilian Christian wa kampuni ya Uchapaji ya Mkuki na Nyota baada kukizindua katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Jumanne Novemba 12, 2019.
*****************
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 12 Novemba, 2019 amezindua kitabu cha maisha binafsi ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa kiitwacho “My Life, My Purpose” (Maisha Yangu, Kusudio Langu).
Sherehe za uzinduzi wa kitabu hicho zimefanyika katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe. Dkt. Ali Hassan Mwinyi na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Wengine ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Majaji Wakuu Wastaafu, viongozi wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Mabalozi, Wabunge, viongozi wastaafu waliofanya kazi na Mhe. Mkapa akiwa Rais, viongozi wa Taasisi mbalimbali na Wakuu wa Mikoa.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Rais Mstaafu Mkapa kwa kuandika kitabu kuhusu maisha yake kuanzia alipozaliwa mwaka 1938 katika Kijiji cha Lupaso, Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara, safari yake ya masomo, siasa na uongozi alipokuwa Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya mwaka 1995 na mwaka 2005, kwa kuwa kitabu hicho kitawasadia Watanzania na watu wengine duniani kujifunza na kufahamu mchango mkubwa alioutoa kwa Taifa la Tanzania na katika Jumuiya ya kimataifa katika masuala ya maendeleo na uongozi.
Mhe. Rais Magufuli amekiri kuwa Mhe. Rais Mstaafu Mkapa ni mfano wake wa kuigwa na amemshukuru kwa mchango wake mkubwa katika safari yake ya siasa na uongozi kuanzia mwaka 1995 alipomnadi katika kampeni za Uchaguzi Mkuu akigombea Ubunge, alipomteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na baadaye Waziri wa Ujenzi, alipokubali ushauri wake akiwa katika nyadhifa hizo na alipomtia moyo katika uamuzi wake wa kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015.
Ametaja moja ya ushauri ulioungwa mkono na Mhe. Rais Mstaafu Mkapa kuwa ni Serikali ya Tanzania kuanza kujenga barabara za lami kwa kutumia fedha za ndani kwa kutenga shilingi Bilioni 1.85 kila mwezi, na kusimamia kwa karibu utendaji wa Wizara hali iliyopelekea aitwe jina la utani la Askari wa Mwamvuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Rais Mstaafu Mkapa kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania na kupiga vita umasikini kwa kuanzisha mikakati mbalimbali ikiwemo Mkakati wa Kukuza na Kuondoa Umasikini Tanzania (MKUKUTA), Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM).
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa na juhudi zilizofanywa na Mhe. Rais Mkapa katika kukuza uchumi, kuondokana na utegemezi na kudumisha amani, na kwamba ni kutokana na hilo hata Serikali ya Awamu ya Tano anayoiongoza inasimamia mwelekeo huo.
Pamoja na kuipongeza Taasisi ya Uongozi kwa kuandika kumbukumbu za viongozi, ameitaka taasisi hiyo kuchapisha kitabu cha maisha binafsi ya Mhe. Rais Mstaafu Mkapa kwa lugha ya Kiswahili ili Watanzania wengi waweze kusoma, na ametoa wito kwa viongozi wengine wakiwemo wa ngazi za chini kuandika vitabu kuhusu maisha yao.
Kwa upande wake Mhe. Rais Mstaafu Mkapa, amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kukubali kuzindua kitabu chake na amempongeza kwa msimamo wake wa kuhakikisha Tanzania inajitegemea hasa katika maendeleo.
Mhe. Rais Mstaafu Mkapa amewashukuru wote walioshiriki katika uandaaji na uchapishaji wa kitabu cha maisha yake binafsi na amesema pamoja na kuandika kuhusu maisha yake, katika kitabu hicho ameeleza jinsi alivyofanya kazi na kumfahamu Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambaye fikra zake bado zipo hai na zina mashiko mpaka sasa.
Uzinduzi wa kitabu cha maisha binafsi ya Rais Mstaafu Mkapa, umekwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 81 ya tangu kuzaliwa kwake, ambapo viongozi waliohudhuria sherehe hizo wamepata nafasi ya kumpongeza, kumtakia afya njema na maisha marefu na pia wameshiriki nae chakula cha mchana kilichoandaliwa kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli.
0 comments:
Post a Comment