Mtendaji Mkuu Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Eng. Peter Ulanga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo kuhusiana na maadhimisho ya miaka 10 ya mfuko huo yanayofanyika jijini Dodoma yakibebwa na kauli mbiu ya "Mawasiliano kwa Wote ni Kichocheo cha Kuufikia Uchumi wa Kati".
MAADHIMISHO YA MIAKA KUMI YA MFUKO WA
MAWASILIANO KWA WOTE (UCSAF)
Mfuko
wa Mawasiliano kwa Wote nchini (UCSAF) unatarajia kufanya maadhimisho ya Miaka
10 tangu kuanzishwa kwake. Maadhimisho hayo ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa
Mfuko ni sehemu ya Utekelezaji wa Kauli Mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya
Kuufikia Uchumi wa Kati. Kauli mbiu katika maadhimisho haya ni Mawasiliano kwa Wote ni Kichocheo cha
Kuufikia Uchumi wa Kati.
Maadhimisho
haya yatafanyika hapa Dodoma kuanzia tarehe 27 Aprili hadi kilele chake tarehe
30 Aprili, 2019 ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mbunge).
Katika
maadhimisho haya, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umeandaa shughuli mbalimbali
katika kipindi cha muda wa maadhimisho, yakiwemo maonesho ya watoa huduma
mbalimbali za mawasiliano nchini ambayo yatafanyika kuanzia tarehe 27 Aprili
hadi siku ya kilele tarehe 30 Aprili 2019. Mfuko unachukua fursa hii kuualika
umma wa wananchi wa Jiji la Dodoma pamoja nanyi waandishi wa habari kuhudhuria maonesho
hayo yatakayofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere (maarufu kama Nyerere
Square) jijini Dodoma.
Sambamba
na maonesho hayo, Mfuko utazindua Klabu za TEHAMA katika Shule za Sekondari za
Dodoma pamoja na Msalato zilizoko Dodoma siku ya tarehe 28 April 2019. Aidha
Mfuko utagawa Kompyuta kwa Wilaya ya Gairo pamoja na kuzindua mnara wa mawasiliano
uliopo wilaya ya Bahi siku ya tarehe 29 Aprili 2019, ikiwa ni kielelezo cha
miradi ambayo inatekelezwa maeneo mengi nchini Tanzania Bara na Visiwani.
Kwa
miongo mingi Sekta ya Mawasiliano imekuwa ikikuwa kwa kasi ndogo katika nyanja
zote za simu, posta na utangazaji. Mabadiliko ya Sekta ya Mawasiliano yalianza
miaka ya 90 ambapo mfumo wa uendeshaji wa sekta ulibadilishwa na kuingiza uwepo
wa wadhibiti wa sekta (Tume ya Mawasiliano na Tume ya Utangazaji) na kuanza
kuingiza ushindani katika sekta ya mawasiliano.
Miaka
10 baadaye mabadiliko zaidi ya kisekta yalifanyika kwa kuunganisha Tume ya
Mawasiliano na Tume ya Utangazaji na kuunda Mamlaka ya Mawasiliano mwaka 2003.
Katika kuongeza ushindani katika soko la mawasiliano lilijitokeza ombwe katika
muundo wa sekta katika ngazi ya kiutendaji. Ombwe hilo lilitokana na nguvu za
ushindani kujikita kupeleka mawasiliano katika maeneo yenye mvuto wa kibiashara
na kuyaacha maeneo ya vijijini na ya mijini yasio na mvuto wa kibiashara.
Serikali ililiona hilo kuanzia mwaka 2003 mpaka mwaka 2006 ambapo sheria ya
kuanzisha Mfuko Mahsusi kwa ajili ya Mawasiliano ilipitishwa na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mfuko huo ulianzishwa kama taasisi ya serikali
inayojitegemea chini ya Wizara inayohusika na mawasiliano. Kanuni za kuanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa
Wote zilisainiwa mwezi Aprili 2009.
Sekta
ya Mawasiliano katika kipindi kirefu cha tabribani miaka 30 iliyopita imepitia
mabadiliko makubwa sana ambapo sekta imetoka kwenye kuwa na kampuni moja ya
umma kabla ya mwaka 1993 ambayo ilikuwa inatoa huduma za simu za mezani, posta
na hata telegramu na telex mpaka kuwa na soko kubwa la ushindani lenye
makampuni makubwa ya simu za mkononi.
Sekta ya mawasiliano imefaidi sana kwa uwepo wa mdhibiti wa mawasiliano
aliyethabiti na kutoa mwongozo ambao umeifanya sekta ya mawasiliano kuwa sekta
inayochangia maendeleo makubwa ya uchumi wa Tanzania.
Mabadiliko
ya kisekta yaliyofanywa na Serikali mwaka 2005 yaliongeza kasi ya ushindani
katika sekta ya mawasiliano na mabadiliko ya aina hiyo yalitokea kwenye sekta
ya utangazaji na sekta ya posta. Kuongezeka kwa ushindani kulisababisha
ushindani wa bei na kufanya gharama kuanza kupungua hata hivyo kutokana na hali
hiyo watoa huduma walichelea kupeleka mawasiliano ya aina zote maeneo ambayo
yataonekana kukosa mvuto wa kibiashara hasa maeneo ya vijijini.
Serikali
ilianzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote mwaka 2006 na kusainiwa na Mheshimiwa
Raisi mwaka 2007. Hata hivyo kanuni za kuanzisha Mfuko zilisainiwa Aprili 2009.
Lengo kuu la kuanzishwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ni kuhakikisha Mtanzania
popote alipo ataweza kupata huduma za uhakika za mawasiliano iwe ni mawasiliano
ya simu za mkononi, utangazaji, huduma za posta au intaneti.
Toka
kuanzishwa kwake Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umejikita kutambua mahitaji ya
mawasiliano nchi nzima, kushirikisha wadau mbali mbali wa mawasiliano nchini,
kushirikisha wananchi katika kutambua na kutatua kero za mawasiliano. Wakati
Mfuko unaanza takriban asilimia 45 tu ya watanzania walikuwa wanaishi katika
maeneo yanayofikiwa na mawasiliano ya simu. Mpaka tunavyoongea leo takriban
asilimia 94 ya watanzania wanaishi kwenye maeneo yanayofikiwa na mawasiliano ya
simu ambapo zaidi ya asilimia 70 ni watumiaji wa huduma za mawasiliano ya
simu. Asilimia 10 imechangiwa na Mfuko
wa Mawasiliano.
Imetolewa na
Eng.
Peter Ulanga
Mtendaji
Mkuu
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote
0 comments:
Post a Comment