Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba akitoa mada mbele ya wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini (hawapo pichani) wakati wa semina ya siku mbili kwa wajumbe hao kutoka kwa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (MB) akikubaliana jambo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Mhe. Dustan Kitandula (kulia) wakati wa semina ya siku mbili kwa wajumbe hao kutoka kwa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakifuatilia kwa umakini uwasilishaji wa taarifa za maendeleo ya miradi ya nishati katika semina ya siku mbili kwa wajumbe hao kutoka kwa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati.
**************
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Dustan Kitandula, Mbuge wa Mkinga mkoani Tanga, wamekutana na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati kupokea taarifa za maendeleo ya miradi mbalimbali katika taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo.
Akiwasilisha miradi ya kipaumbele ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Kapuulya Musomba alieleza kwamba TPDC imeweka kipaumbele katika vipengele muhimu ikiwa ni pamoja na; kuunganisha wateja wapya wa viwandani na majumbani, kuwekeza zaidi katika utafiti na uendelezaji wa mafuta na gesi, kushiriki katika mradi wa gesi ya kimiminika (LNG), kuharakisha utekelezaji wa mradi wa mafuta ya kimkakati (SPR), kuwajengea uwezo wataalamu wa Shirika la TPDC pamoja na kuendelea kutoa taarifa sahihi na kwa wakati juu ya maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi.
Mhandisi Musomba alieleza kwamba katika kukabiliana na changamoto ya mtaji mdogo wa biashara, TPDC imejipanga kushirikiana na sekta binafsi katika mfumo wa PPP (Public Private Partnership) katika kutekeleza miradi ya usambazaji wa gesi asilia hapa nchini.
“Usambazaji wa gesi asilia hapa nchini unafanywa kulingana na Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi Asilia wa mwaka 2016” anaeleza zaidi Mhandisi Musomba.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa semina ya siku mbili kwa Kamati hiyo ya Bunge, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (MB) alieleza mabadiliko ya majukumu ya TPDC kama yalivyoainishwa katika sheria ya Petroli ya 2015 [Petroleum Act, 2015) ambapo TPDC imetambulika kama Shirika la Taifa la Mafuta (National Oil Company-NOC).
Waziri Kalemani alieleza kwamba TPDC sasa ina jukumu la kujiendesha kibiashara na kusimamia maslahi na ushiriki wa kibiashara wa Serikali katika miradi ya utafiti, uendelezaji, uzalishaji na usambazaji wa mafuta na gesi hapa nchini.
Waziri Kalemani alisema “Sheria mpya ya petroli pamoja na mambo mengine inaitaka TPDC iachane na uendeshaji ule wa zamani na kujiendesha kama shirika la kibiashara linalotengeneza faida na kukuza mtaji”.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula aliipongeza TPDC kwa jitihada za kusambaza gesi majumbani na viwandani na kuwataka kuongeza kasi ya usambazaji gesi na utafutaji masoko ili kutumia vema bomba kubwa la gesi linalotoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Kitandula aliongeza kwamba kuna fursa kubwa ya matumizi ya gesi asilia hapa nchini na TPDC iziangalie kwa jicho la tatu ili kuweza kufaidika nazo.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ndio yenye jukumu la kuishauri bunge juu ya masuala yahusuyo sekta ya nishati na madini.
Semina hiyo ya siku mbili ililenga kuangazia maendeleo katika sekta ya nishati na madini pamoja na changamoto zinazohitaji kutatuliwa ili sekta iweze kutoa matokeo chanya zaidi katika uchumi wa Taifa.
0 comments:
Post a Comment