Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Slaa (wapili kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila (wapili kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela wakizindua rasmi maadhimisho ya miaka 30 ya Benki ya CRDB katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Posta jijini Dar es Salaam tarehe 14 Februari 2025.
Dar es Salaam – Benki ya CRDB yatangaza mpango wa kupanua huduma zake hadi Dubai. Hatua hii inaiweka Benki hiyo kwenye ramani kama taasisi ya kwanza ya kifedha kutoka Afrika Mashariki kupanuka nje ya bara la Afrika, jambo linalotengeneza fursa zaidi za biashara na uwekezaji.
Taarifa hiyo imetolewa wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 30 ya benki hiyo, ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alimweleza Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Jerry Slaa, kuhusu mkakati huo muhimu.

“Safari yetu ya miaka 30 imejaa ustahimilivu, mabadiliko, na ubunifu. Teknolojia imekuwa mhimili mkubwa wa ukuaji wetu, ikituruhusu kupanua wigo wa huduma zetu hadi nje ya Tanzania. Leo hii, tunajivunia kuwa benki inayoongoza katika kutoa suluhisho za kifedha zinazochochea ujumuishi wa kiuchumi na maendeleo ya jamii,” alisema Nsekela.
Mpango wa Benki ya CRDB kutanua wigo wa huduma zake hadi Dubai unatokana na nafasi yake kama kitovu cha biashara na fedha duniani. Upanuzi huu utaunganisha biashara za Afrika Mashariki na masoko mapana zaidi, na kufungua milango kwa fursa mpya za maendeleo.

Nsekela pia alieleza uimara wa kifedha wa benki hiyo, akieleza kuwa matokeo ya fedha yasiyokaguliwa 2024 yanayoonyesha kuwa Benki ya CRDB inaongoza kwa ukubwa nchini. Kwa sasa, benki ina jumla ya mali zenye thamani ya Shilingi trilioni 16.6, amana za wateja za Shilingi trilioni 10.9, na mikopo iliyotolewa yenye thamani ya Shilingi trilioni 10.4.
Aidha, alitoa shukrani za dhati kwa wateja, wanahisa, Serikali, washirika, na wadau wote kwa kuwa sehemu ya mafanikio ya Benki ya CRDB kwa miaka 30 iliyopita. “Tumeweza kufanikisha safari hii kwa sababu ya imani yenu na msaada wenu usioyumba. Tunathamini sana mchango wenu na tunaahidi kuendelea kuwahudumia kwa ubora zaidi huku tukipanua huduma zetu kimataifa.”

Kwa upande wake, Mheshimiwa Jerry Slaa aliipongeza Benki ya CRDB kwa mafanikio yake makubwa na mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania. “Kufikisha miaka 30 ya ubora katika sekta ya fedha ni jambo la kujivunia.
Benki hii imekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wetu, na upanuzi wake hadi Dubai ni uthibitisho wa nafasi yake kama benki kiongozi. Hatua hii inaendana na dira ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika biashara za kimataifa.”

Waziri pia alitambua mchango wa CRDB Bank kama mlipa kodi mkubwa na ikiongoza kutoa ajira kwa wa maelfu ya Watanzania, ikiwa na zaidi ya wafanyakazi 4,000. “Mchango wenu katika sekta ya fedha na maendeleo ya taifa ni mkubwa. Itakuwa vyema kuona benki hii ikitunukiwa heshima ya kitaifa kwa mchango wake katika Tanzania na Afrika Mashariki.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay, alieleza kuwa benki hiyo ilianzishwa kwa nia ya kuimarisha sekta ya fedha nchini kupitia mageuzi ya kimkakati. “Kwa miaka yote hii, tumeendelea kupanua huduma za kifedha na kuchangia ukuaji wa uchumi kwa ushirikiano wa karibu na Serikali,” alisema Dkt. Ally.

Aliongeza kuwa utendaji mzuri wa kifedha wa Benki ya CRDB umeendelea kuongeza thamani kwa wanahisa wake. “Tangu mwaka 2010, bei ya hisa zetu imeongezeka kutoka TZS 115 hadi TZS 700, ikiwa ni ongezeko la 509%. Sera yetu ya gawio inahakikisha angalau 30% ya faida inarejeshwa kwa wanahisa kila mwaka, ambapo mwaka jana gawio lilifikia TZS 50 kwa hisa, ongezeko la 525% tangu benki ilipoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) mwaka 2009.”
Akielezea mustakabali wa benki hiyo, alisema Benki ya CRDB itaendelea kutumia teknolojia na ushirikiano wa kimkakati kupanua huduma zake kimataifa huku ikiimarisha uongozi wake katika Tanzania, Burundi, na DRC. Kuingia Dubai ni mwanzo wa enzi mpya ya ujumuishi wa kifedha, ambapo biashara na wawekezaji wa Afrika Mashariki wataweza kufanikisha biashara zao kwa urahisi zaidi katika soko la kimataifa.


Sherehe hizi zilipewa mvuto wa kipekee kwa onyesho la kihistoria la ndege zisizo na rubani (drone light show) lililopamba anga la Dar es Salaam kwa mandhari ya kuvutia, na kuwasisimua wakazi kutoka kila kona ya jiji.

Akizungumza katika maadhimisho haya, Mkurugenzi wa Mwawasiliano wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa alieleza kuwa katika mwaka huu wa maadhimisho, benki hiyo itaendesha shughuli mbalimbali za kushirikiana na wateja, wanahisa, jamii, na wadau wake wote ili kuendelea kujenga ustawi wa pamoja.


0 comments:
Post a Comment