Na: Mwandishi Wetu, Tanga
Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Ummy Mwalimu (CCM) ametoa rai kwa wananchi wa Jimbo la Tanga Mjini kujitoleza kwa wingi katika zoezi la kitaifa la uboreshaji wa daftari la wapigakura ili waweze kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuchangua viongozi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, 2025.
Rai hiyo ameitoa wakati akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hii kuhusiana na zoezi la uboreshaji na uandikishaji wapigakura linaloendelea mkoani Tanga ambapo kwa Jimbo la Tanga Mjini, zoezi hilo linaanza Februari 13 hadi 19, 2025 katika vituo mbalimbali kwenye kata zote 27 za Jimbo la Tanga Mjini.
Ummy Mwalimu amewahimiza wananchi kutopoteza fursa hiyo kwani njia pekee ya kupata viongozi bora inaanzia katika kujiandikisha na kumalizika kwa kupiga kura siku ya uchaguzi.
"Yale maendeleo ambayo wananchi wa Tanga Mjini tunayataka yanaanzia katika kujiandikisha na mwisho wa siku kupiga kura kuchangua viongozi bora. Niwasihi wananchi wote kutopoteza fursa hii ambayo itaamua mwelekeo wa maendeleo wayatakayo," amesema Ummy Mwalimu.
Katika hatua nyingine, Ummy Mwalimu amewahamasisha wananchi ambao wamehama makazi kutoka sehemu moja kwenda nyingine, waliopoteza kadi au ambao kadi zao zimeharibika, walio na umri wa miaka 18 au zaidi na ambao hadi kufika siku ya uchaguzi watakuwa wamefikisha miaka 18, wanaotaka kuboresha taarifa zao mathalani majina, wajitokeze kujiandikisha katika vituo vya kujiandikisha kuanzia saa mbili kamili asubuhi hadi saa kumi na mbili kamili jioni.
Huu ni mwendelezo wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuboresha na kuandikisha wapigakura ili kuwapa fursa wananchi kujiandikisha ili kutopoteza fursa ya kuchangua viongozi kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment