Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amemtumia salamu za rambirambi
Mkuu wa Mkoa wa Tanga kufuatia vifo vya watu 12 vilivyosababishwa na kuzama kwa
boti waliyokuwa wakisafiria kutoka Tanga kwenda Pemba.
Ajali hiyo
imetokea usiku wa kuamkia leo tarehe 10 Januari, 2017 katika kisiwa cha Jambe kilichopo katika bahari ya Hindi umbali mfupi
kutoka Tanga Mjini, ambapo pamoja na vifo vya watu hao watu wengine 33
wamenusurika na 25 kati yao wamelazwa katika Hospitali ya Bombo Mkoani Tanga.
"Nimeshtushwa
na kusikitishwa sana na vifo vya watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika
ajali hii ya kuzama boti, tumepoteza wapendwa wetu, watoto wetu na watu wazima
ambao kwa hakika familia zao ziliwategemea katika maisha ya kila siku, nakuomba
Ndg. Mkuu wa Mkoa unifikishie pole nyingi kwa familia za Marehemu wote na jamaa
zao" amesema Dkt. Magufuli katika
salamu hizo.
Aidha, Rais Magufuli
amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na pia amewataka wote
walioguswa na vifo hivyo kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi
hiki cha huzuni ya kuondokewa na jamaa zao.
Dkt. Magufuli pia
amewatakia matibabu mema majeruhi wote walionusurika katika ajali hiyo ili
wapone haraka, warejee katika familia zao na waendelee na ujenzi wa Taifa.
"Bwana ametoa
na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe, Amen"
Amemalizia Rais Magufuli.
0 comments:
Post a Comment