Waziri wa
Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo,Nape Nnauye (kulia) akieleza jambo kwa Waziri
wa Sanaa na Utamaduni wa Afrika Kusini Ndg. Nathi Mthehwa(kushoto)
ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi kwa siku tatu yenye lengo la kuimarisha
ushirikiano baina ya nchi hizo kupitia Sanaa na Utamaduni ikiwemo kuhifadhi
historia ya ukombozi wa Afrika ya Kusini leo Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa
Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akiongea na waandishi wa habari (hawapo katika
Picha) leo Jijini Dar es Salaam kuhusu ziara ya Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa
Afrika Kusini, Nathi Mthehwa
ambaye yupo nchini kwa siku tatu kwa lengo la kuimarisha ushirikiano
baina ya nchi hizo kupitia sekta ya Sanaa na Utamaduni ikiwemo kuhifadhi
historia ya ukombozi wa Afrika Kusini.
Ujumbe uliofuatana na mawaziri hao ukisikiliza mazungumzo.
Na Genofeva Matemu -
WHSUM
SERIKALI ya Tanzania
itaendelea kuweka historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika kwa kuhifadhi
kumbukumbu zote huku ikitunza na kuweka alama maeneo ambayo yalitumika wakati
wa kupigania Uhuru wa Bara la Afrika na kutunza makaburi ya wapigania uhuru hao
pamoja na kuyafanya kuwa ya kihistoria.
Hayo yamesemwa leo
Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alipokutana na Waziri wa Utamaduni na Sanaa wa Afrika Kusini, Nathi Mthehwa aliyeko nchini kwa ziara ya siku tatu kwa lengo la kuimarisha
uhusiano wa nchi hizo mbili katika sekta ya Utamaduni na Sanaa.
“Tumeanza kuandika historia ya Ukombozi wa
Bara la Afrika kwa kuhoji baadhi ya wanaharakati walioshiriki katika kuwasaidia
wapigania uhuru kuanzisha vyama vyao vya ukombozi ambapo historia hii
itahifadhiwa kwa njia ya sauti na picha lakini pia tutaendelea kutunza kumbukumbu
zote tutakazozipata na kuwekea alama maeneo ambayo yalitumika wakati wa kupigania
uhuru” amesema, Nape.
Aidha, Nape
amesema kuwa makubaliano yaliyosainiwa mwaka 2011 kati ya Tanzania na Afrika ya
Kusini kufuta Visa ya kusafiria kati ya nchi hizo mbili yameleta mabadiliko makubwa katika eneo la Sanaa
nchini kwani wasanii wamekua wakitumia fursa hiyo kwenda Afrika ya Kusini
kuandaa kazi zao na kuzifanya kuwa na ubora zaidi.
Kwa upande wake
Waziri wa Utamaduni na Sanaa wa Afrika Kusini , Nathi Mthehwa ameishukuru
Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili
na kuthamini mchango uliofanywa na Tanzania katika kukomboa nchi ya Afrika Kusini.
Pamoja na hayo,
Mthethwa ameahidi kuendeleza ushirikiano ulipo na kuthamini maendeleo yaliyopo
kwenye maeneo ya Utamaduni na Sanaa kwa kuhakikisha kuwa mafanikio ya Sekta za
Ubunifu ndani ya Afrika Kusini yanakua sehemu ya mafanikio ndani ya nchi ya
Tanzania.
Ziara hii inaangalia
namna nchi hizi mbili zinaweza kuimarisha makubaliano ya mwaka 2011, katika maeneo
mengine ya mashirikiano kama vile upande wa tasnia ya filamu ambapo Afrika Kusini imekua ikifanya vizuri ikiwemo kusimamia haki za wasanii kwa kutengeneza
mifumo ya kisheria ya kulinda haki za ubunifu na kuongeza mahusiano ya nchi hizo mbili.
Waziri huyo atatembelea Mkoa wa Morogoro kwenye kambi ya
wapigania Uhuru wa Afrika Kusini Mazimbu, Dakawa pamoja na Bagamoyo ambapo
kulikua na kambi yao,pamoja na baadhi ya maeneo Jijini Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment