Nafasi Ya Matangazo

November 18, 2016



Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo,Nape Nnauye (kulia) akieleza jambo kwa Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa   Afrika Kusini Ndg. Nathi Mthehwa(kushoto) ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi kwa siku tatu yenye lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo kupitia Sanaa na Utamaduni ikiwemo kuhifadhi historia ya ukombozi wa Afrika ya Kusini leo Jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Nape Nnauye  akiongea na waandishi wa habari (hawapo katika Picha) leo Jijini Dar es Salaam kuhusu ziara ya Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Afrika Kusini, Nathi Mthehwa  ambaye yupo nchini kwa siku tatu kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo kupitia sekta ya Sanaa na Utamaduni ikiwemo kuhifadhi historia ya ukombozi wa Afrika Kusini.

 Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa   Afrika Kusini, Nathi Mthehwa (kulia) akizungumza katika mkutano huo. Kulia ni Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Nape Nnauye .


 Ujumbe uliofuatana na mawaziri hao ukisikiliza mazungumzo.
Na Genofeva Matemu - WHSUM
SERIKALI ya Tanzania itaendelea kuweka historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika kwa kuhifadhi kumbukumbu zote huku ikitunza na kuweka alama maeneo ambayo yalitumika wakati wa kupigania Uhuru wa Bara la Afrika na kutunza makaburi ya wapigania uhuru hao pamoja na kuyafanya kuwa ya kihistoria.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alipokutana na Waziri wa Utamaduni na Sanaa wa Afrika  Kusini, Nathi Mthehwa aliyeko nchini kwa ziara ya siku tatu kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili katika sekta ya Utamaduni na Sanaa.

 “Tumeanza kuandika historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika kwa kuhoji baadhi ya wanaharakati walioshiriki katika kuwasaidia wapigania uhuru kuanzisha vyama vyao vya ukombozi ambapo historia hii itahifadhiwa kwa njia ya sauti na picha lakini pia tutaendelea kutunza kumbukumbu zote tutakazozipata na kuwekea alama maeneo ambayo yalitumika wakati wa kupigania uhuru” amesema, Nape.

Aidha, Nape amesema kuwa makubaliano yaliyosainiwa mwaka 2011 kati ya Tanzania na Afrika ya Kusini kufuta Visa ya kusafiria kati ya nchi hizo mbili yameleta  mabadiliko makubwa katika eneo la Sanaa nchini kwani wasanii wamekua wakitumia fursa hiyo kwenda Afrika ya Kusini kuandaa kazi zao na kuzifanya kuwa na ubora zaidi.

Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni na Sanaa wa Afrika Kusini ,  Nathi Mthehwa ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili na kuthamini mchango uliofanywa na Tanzania katika kukomboa nchi ya Afrika Kusini.

Pamoja na hayo,  Mthethwa ameahidi kuendeleza ushirikiano ulipo na kuthamini maendeleo yaliyopo kwenye maeneo ya Utamaduni na Sanaa kwa kuhakikisha kuwa mafanikio ya Sekta za Ubunifu ndani ya Afrika Kusini yanakua sehemu ya mafanikio ndani ya nchi ya Tanzania.

Ziara hii inaangalia namna nchi hizi mbili zinaweza kuimarisha makubaliano ya mwaka 2011, katika maeneo mengine ya mashirikiano kama vile upande wa tasnia ya filamu ambapo Afrika Kusini imekua ikifanya vizuri ikiwemo kusimamia haki za wasanii kwa kutengeneza mifumo ya kisheria ya kulinda haki za ubunifu na kuongeza mahusiano ya  nchi hizo mbili.

Waziri huyo  atatembelea Mkoa wa Morogoro kwenye kambi ya wapigania Uhuru wa Afrika Kusini Mazimbu, Dakawa pamoja na Bagamoyo ambapo kulikua na kambi yao,pamoja na baadhi ya maeneo Jijini Dar es Salaam.
Posted by MROKI On Friday, November 18, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo