Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba akiangalia eneo
lililokuwa likitumiwa na Jema Sitalike Project ambao walizuiwa kuendelea na
shughuli za uchenjuaji wa dhahabu kutokana na kutokuwa na vibali. Wengine
katika picha ni pamoja Mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Jenerali Mstaafu Raphael
Muhuga
Mashimo yaliyokuwa
yakitumiwa na Jema Sitalike Project ambao walizuiwa kuendelea na shughuli za
uchenjuaji wa dhahabu kutokana na kutokuwa na vibali, yakiwa yameachwa wazi
hali inayotishia usalama wa wananchi wanaozuka maeneo hayo. Waziri Makamba
ameagiza kusimamishwa kwa shughuli za Mradi wa Jema ambao kwa sasa wamehamishia
shughuli zao Mkoani Mwanza na kuwataka kuchukua hatua za haraka kufunika mashimo
yaliyopo Sitalike - Katavi
Viboko Katika
Hifadhi ya Taifa ya Katavi wakiwa wanaathirika kutokana na upungufu wa maji
katika Mto Katuma. Waziri Makamba ametangaza hatua za haraka na za muda mrefu
za kurejesha mto huo katika hali yake ya awali.
Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba amesema kuwa
uharibifu wa Mazingira katika Mto Katuma ni tishio kubwa kwa uhai wa Hifadhi ya
Taifa ya Katavi na wakazi wa Mkoa huo.
Akiwa katika mwendelezo
wa ziara yake ya siku 16 kutembelea Mikoa mbalimbali hapa nchini, Waziri
Makamba amesema kuwa Mto Kasuma uko hatarini kutoweka kutokana na ongezeko la
shughuli za binadamu, wingi wa mifugo,
Uchimbaji wa madini, ukataji wa miti na uchepushaji wa maji
kunakopelekea kupoteza mtiririko wa maji yenyewe.
Waziri Makamba
amesema ni vema kuwa na mikakati na hatua za haraka na zile za muda mrefu ikiwa
ni pamoja na kufanya sensa ya mifugo ili kuweza kujua Mkoa una mifugo kiasi
gani na kuainisha maeneo ya malisho. "Zoezi hili si hiari, ni lazima na
takwa la kisheria' Makamba alisisitiza.
Imependekezwa pia
kufanyika kwa Ubomoaji wa mabanio yanayokinga maji kama hatua ya haraka ili
maji yaweze kutiririka kwa wingi katika kipindi hiki cha kiangazi, na kuagiza
kufanyika kwa doria za mara kwa mara ili kubaini watu wanaokiuka taratibu hizo.
Waziri Makamba pia
amezitaka Mamlaka za bonde kutimiza wajibu wao kwa kutoa vibali stahiki
kulingana na ujazo wa maji uliopo katika maeneo yao ili kujenga usawa wa
matumizi sahihi ya rasilimali maji. ' Mamlaka za bonde zisitoe vibali ofisini
na operesheni ifanyike kwa wote wasio na vibali" Alisema Waziri Makamba.
Pia, Waziri Makamba
ameagiza kufanyika kwa Tathimini ya athari kwa mazingira kwa Mto Kasuma na kuuagiza
uongozi wa Mkoa wa Katavi kuainisha baadhi ya maeneo ambayo yatatangazwa kama
maeneo nyeti ili kunusuru mazingira ya Katavi na ustawi wa Mto Katuma.
"Kuwe na tozo
ya uharibifu wa Mazingira na tozo hiyo iendane na kiwango cha uharibifu
atakachofonya muhusika"
Akiongea na Wadau wa
Mazingira katika Ukumbi wa Maji Mkoani Katavi Waziri Makamba amekumbusha
watumishi wa Umma Nchini kuwa na nidhamu na uwajibikaji wa dhati na kusisitiza
kuwa hakuna muda wa kubembelezana. "Fanyeni kazi kwa weledi, nidhamu na
uadilifu" alisema Makamba.
Katika hatua
nyingine Waziri Makamba ametembelea eneo ulipokuwa mradi wa uchenjuaji wa
dhahabu wa Jema Sitalike Project ambao ulikua ukifanya shughuli zake bila
kibali cha Wizara ya Nishati na Madini na Baraza la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Waziri Makamba
ameagiza kusimamishwa kwa shughuli za Mradi wa Jema ambao kwa sasa wamehamishia
shughuli zao Mkoani Mwanza na kuwataka kuchukua hatua za haraka kufunika
mashimo yaliyopo Sitalike - Katavi ili kunusuru uhai wa viumbe vinavyozunguka
maeneo ya Sitalike.
Waziri Makamba yuko
Mkoani Katavi kwa ziara ya kikazi na hii leo amekutana na Viongozi wa Vikundi
vya Mazingira, katembelea eneo lilikokuwa na shughuli za Uchimbaji wa Madini na
chanzo cha Mto Katuma.
0 comments:
Post a Comment