JUMLA ya kikosi cha watu 35 ambao ni wachezaji na viongozi wa Mouloudia Olympique Bejaia au maarufu MO Béjaïa
kutoka Algeria, wametua Dar es Salaam, usiku wa kuamkia Agosti 9, 2016 na
imefikia Hoteli ya Ledger Plaza, iliyoko Kunduchi Beach nje kidogo ya jiji la
Dar es Salaam.
Timu hiyo imekuja kucheza na Young Africans ya Dar es Salaam, katika
mchezo wa nne wa hatua ya Nane Bora kuwania Kombe la Shirikisho Barani Afrika
utakaofanyika Jumamosi Agosti 13, 2016 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Licha ya kwamba Young Africans kuwa na pointi moja, bado ina nafasi ya
kushika nafasi za juu katika kundi la A ambalo msimamo wake unaongozwa na TP
Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku Mo Bejaia ya Algeria na
Medeama ya Ghana, zina pointi tano kila moja. Wakati Young Africans wanacheza
na Mo Bajaia iliyoshinda mchezo wa kwanza huko Algeria, Medeama itakipiga na TP
Mazembe.
Mchezo wa Young Africans dhidi ya Mo Bejaia utachezeshwa na waamuzi
kutoka Ethiopia ambako katikati atakuwa Bamlak Tessema Weyesa akisaidiwa na
Kindie Mussie mstari upande wa kusini na Temesgin Samuel Atango katika mstari
wa Kaskazini upande wa wakati Mwamuzi wa Akiba atakuwa Haileyesus Bezezew
Belete.
Kamishna wa mchezo atakuwa Gaspard Kayijuka kutoka Rwanda wakati Desire
Gahuka wa Burundi atasimamia ufanisi wa waamuzi wa mchezo na Mratibu Mkuu wa
mchezo atakuwa Isam Shaaban kutoka Sudan. Mratibu huyo anatarajiwa kuwasili leo
Agosti 10, 2016 wakati waamuzi watatua kesho Agosti 11, 2016 na msimamizi wa
waamuzi atatua Ijumaa Agosti 12, 2016.
Kiingilio katika mchezo huo kitakuwa ni Sh 3,000 kwa mzungunguko kwa
maana ya viti vya kijani, bluu na chungwa wakati Viti Maalumu vyenye hadhi ya
daraja B na C kiingilio kitakuwa Sh 10,000 wakati A kiingilio kitakuwa ni Sh
15,000 kwa mujibu wa Waratibu wa Young Africans.
0 comments:
Post a Comment