Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akiwajulia hali watu mbalimbali
wanaopata huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mount Meru, wakati
alipofanya kwa ziara ya kustukiza, kukagua huduma mbalimbali Hospitalini hapo.
Tarehe 28 Septemba.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akikagua mazingira wakati akitembea kuelekea katika Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, kwa ziara ya kustukiza leo Septemba 28, 2026.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akisalimiana na wananchi
mbalimbali wa Jiji la Arusha, wakati akitembea kuelekea katika Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa ya Mount Meru, kwa ziara ya kustukiza. Tarehe 28 Septemba 2026.
***************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ametembelea Hospitali ya Rufaa
ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, kujionea hali ya utoaji wa huduma za afya kwa
wananchi pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili wagonjwa na watumishi
wa hospitali hiyo.
Mara baada ya kuwasili
hospitalini hapo, Makamu wa Rais amepokelewa na viongozi pamoja na watumishi wa
hospitali, ambapo taarifa fupi ilitolewa kuhusu maendeleo, utendaji na huduma
zinazotolewa, kabla ya kutembelea wodi mbalimbali na kuzungumza na wananchi
wanaopata huduma hospitalini hapo.
Akizungumza na wananchi
waliolazwa hospitalini hapo, Mhe. Ndejembi aliwapa pole kutokana na maradhi
yanayowakabili na kuwafikishia salamu za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku akiwahakikishia kuwa Serikali
itaendelea kuipa sekta ya afya kipaumbele na kuboresha huduma zinazotolewa katika
vituo vya afya nchini.
Akiwa katika Wodi ya wazazi,
Makamu wa Rais alieleza kufurahishwa kuwaona akina mama waliojifungua salama
pamoja na watoto wao wakiwa na afya nzuri, akibainisha kuwa Serikali itaendelea
kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto ikiwa ni sehemu ya juhudi za
kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi pamoja na vifo vya watoto.
Alisema jitihada hizo
zinaendana na dhamira ya Rais Samia ya kuhakikisha huduma bora na salama za
afya ya uzazi zinawafikia wanawake na watoto katika maeneo mbalimbali nchini,
sambamba na nafasi yake katika kusukuma mbele ajenda ya kupunguza vifo vya mama
na mtoto barani Afrika.
Katika ziara hiyo, Makamu wa
Rais pia alipata fursa ya kuzungumza ana kwa ana na baadhi ya wagonjwa kuhusu
huduma zinazotolewa hospitalini hapo.
Wagonjwa hao walieleza
kuridhishwa na huduma wanazopatiwa, huku baadhi yao wakitaja kushindwa kulipa
gharama za matibabu. Kufuatia changamoto hiyo, Makamu wa Rais aliwezesha
kulipwa kwa gharama za matibabu za baadhi ya wagonjwa waliokuwa wamekwama
kutokana na kutokuwa na uwezo wa kulipa, hatua iliyowapa unafuu wagonjwa hao
pamoja na familia zao.
Ziara hiyo imempa Makamu wa
Rais nafasi ya kujionea moja kwa moja huduma zinazotolewa katika Hospitali ya
Mount Meru, kusikiliza wananchi wanaozitumia na kufahamu changamoto
zinazowakabili, huku akisisitiza kuendelea na hatua za kuboresha upatikanaji na
ubora wa huduma za afya nchini.
Katika hatua nyingine, Makamu
wa Rais alitembelea maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha, kuwasalimu wananchi na
kujionea hali ya mazingira mkoani humo.
0 comments:
Post a Comment