Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa pili kulia) akikagua eneo la mpaka katika Msitu wa Hifadhi wa Sayaka katika Kijiji cha Bugatu, Wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza hivi karibuni. Anayeongoza utambuzi wa mpaka huo ni Afisa Misitu na Nyuki TFS Wilaya ya Magu, Ayoub Mikae (wa tatu kulia). Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Magu, Boniventure Kiswaga. Eng. Makani aliahidi kwa niaba ya Serikali kupitiwa upya maeneo yoye ya Hifadhi yenye migogoro nchini kwa ajili ya kutafutiwa suluhu ya kudumu.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa sita kushoto) akiwa na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Magu na baadhi ya Wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Msitu wa Sayaka wakikagua mpaka wa hifadhi hiyo hivi karibuni. Kinachoonekana mbele yao ni Kigingi cha mpaka kinachodaiwa kusogezwa mbele na wananchi wa maeneo hayo kwa ajili ya kumega eneo la Hifadhi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kulia) akizungumza na wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Msitu wa Sayaka katika Kijiji cha Bugatu Wilayani Magu Mkoani Mwanza hivi karibuni. Aliahidi kwa niaba ya Serikali kupitiwa upya maeneo yoye ya Hifadhi yenye migogoro nchini na kutafutiwa suluhu ya kudumu.
Naibu Waziri Maliasili , Eng. Ramo Makani (kulia) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Bugatu, Wilaya ya Magu, Mkoani Mwanza hivi karibuni wakati akikagua ramani ya Hifadhi ya Msitu wa Sayaka kubaini maeneo ya mpaka yenye mgogoro. Eng. Makani aliahidi kwa niaba ya Serikali kupitiwa upya maeneo yoye ya Hifadhi yenye migogoro nchini kwa ajili ya kutafutiwa suluhu ya kudumu
Mwananchi wa Kijiji cha Salama kilichopo kandokando ya Hifadhi ya Msitu wa Sayaka Wilayani Magu, Charles Kassandiga (kushoto) akitoa ombi kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho la kupatiwa maeneo ya kulima na kufuga kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kulia). Eng. Makani aliahidi kwa niaba ya Serikali kupitiwa upya maeneo yoye ya Hifadhi yenye migogoro nchini na kutafutiwa suluhu ya kudumu.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kushoto) akiongoza kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama cha Wilaya ya Magu alipotembelea Wilayani humo hivi karibuni kuona eneo la mgogoro katika Hifadhi ya Msitu wa Sayaka ambapo aliahidi kwa niaba ya Serikali kupitiwa upya maeneo yoye ya Hifadhi yenye migogoro nchini na kutafutiwa suluhu ya kudumu.
NA HAMZA TEMBA - WMU
_____________________________________
Serikali kupitia
Wizara ya Maliasili na Utalii imeahidi kupitia upya maeneo yote ya Hifadhi
nchini yenye migogoro ya ardhi kwa ajili ya kuyatafutia suluhu ya kudumu kwa
kutumia mbinu shirikishi.
Hayo yamesemwa
jana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Eng. Ramo Makani wakati akizungumza na
Wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Msitu wa Sayaka katika Kijiji cha
Busega Wilayani Magu Mkoani Mwanza.
Eng. Makani
alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano imekusudia kubadilisha mfumo wa utendaji
Serikali ambapo kwenye utatuzi wa migogoro iliyopo kwenye maeneo ya hifadhi
nchini itatatuliwa kwa kuwashirikisha wananchi wa maeneo husika na kuweka
kumbukumbu sahihi za makubaliano kufikia suluhu ya kudumu.
“Maeneo yote
yenye migogoro tunaenda kuyapitia upya, tukija kwenye utatuzi tutawashirikisha
wananchi kupitia Serikali zao za Vijiji ambazo wajumbe wake watahusika kwenye
makubaliano kwa kuzingatia umuhimu na faida za Uhifadhi lakini huku
tukihakikisha tunajibu kero zinazowakabili” Aliesema Eng. Makani.
Aliongeza kuwa
wakati wa kutatua migogoro hiyo yataainishwa maeneo kwa ajili ya shughuli za ufugaji
na kilimo kuepusha muingiliano kati ya wakulima na wafugaji pamoja na kuepusha
uvamizi kwenye maeneo ya Hifadhi yaliyoainishwa, utaratibu huo utazingatia sheria,
kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya Serikali.
Awali
akizungumzia mgogoro wa Hifadhi ya Msitu wa Sayaka, Eng. Makani alisema kuwa, uamuzi
wa kufika katika eneo hilo la mgogoro ni kuona uhalisia kabla ya kuchukuliwa
hatua za kumaliza mgogoro huo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali
aliyoitoa bungeni hivi karibuni kwa Mbunge wa Jimbo la Magu, Boniventure
Kiswaga.
Katika mgogoro
huo wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi hiyo walitoa malalamiko yao kwa
Naibu Waziri Makani kuwa maofisa wa TFS wamekuwa wakisogeza vigingi vya mpaka
wa eneo hilo kumega maeneo ya vijiji bila kuwashirikisha. “Sio kwamba tunapinga
Uhifadhi, lakini tunauliza kwanini vigingi vinahama kila mwaka kusogelea maeneo
yetu” Alihoji Mwanyekiti wa Kijiji cha Bugatu, Charles Kusenza.
Akijibu
malalamiko hayo Afisa Misitu na Nyuki wa TFS Wilaya ya Magu, Ayoub Mikae
alisema kuwa, kilichokuwa kinafanyika sio kusogeza vigingi bali na kuimarisha
vigingi vilivyokuwepo ambapo utambuzi wake ulifanyika kitaalam kwa kutumia GPS.
Aliongeza kuwa baadhi ya wananchi wasio waadilifu walidaiwa kusogeza vigingi
vya mpaka wa Hifadhi hiyo ili wapate eneo la kulima jambo lililoleta taswira
tofauti wakati wa kufanya marekebisho sahihi kwa kutumia mtambo wa GPS uliosaidia
kubaini mpaka asilia.
Ayoub alisema
kuwa sababu ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu Sayaka ilikuwa ni kuhifadhi uoto
wa asili, kutunza vyanzo vya maji na kuhifadhi samaki wa Ziwa Victoria kwa kuwa
mto uliopo katika hifadhi hiyo unapeleka maji Ziwa Victoria.
Baada ya
kusikiliza hoja mbalimbali za wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi hiyo katika
mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Bugatu, Eng. Makani alisema kuwa tatizo
kubwa aliloliona katika mgogoro huo ni changamoto za Uhifadhi ikiwemo uelewa
hafifu wa baadhi ya wananchi juu ya umuhimu wa uhifadhi, ushirikishwaji hafifu wa
wananchi kwenye uwekaji wa vigingi na baadhi ya wananchi kuchanganya vigingi
vya hifadhi ya maji na hifadhi ya Msitu, changamoto ambazo alisema zitazingatiwa
kwa kina wakati wa utatuzi wa mgogoro huo.
Alisema kuwa “Tunahitaji
uhifadhi endelevu, peke yetu bila wananchi hatuwezi, tunahitaji uhifadhi
rafiki, tukiwa na uelewa wa pamoja juu ya umuhimu wa uhifadhi na tukajibu kero
zenu mtatusaidia kulinda na kuhifadhi Maliasili zetu”.
Kwa upande wa Wananchi
wa vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo waliopewa fursa ya kuchangia na kuuliza
maswali kwenye mkutano huo walipaza sauti zao kuiomba Serikali kupitia Naibu
Waziri huyo kuwasaidia maeneo ya kufuga na kulima kutokana na ufinyu wa maeneo
uliosababishwa na ongezeko kubwa la watu. Naibu Waziri Makani Aliahidi kwa
niaba ya Serikali kupitiwa upya maeneo yoye ya Hifadhi nchini yenye
migogoro na kuyatafutiwa suluhu ya kudumu kwa kuzingatia sheria, kanuni,
taratibu na miongozo mbalimbali ya Serikali.
0 comments:
Post a Comment