Marekani itatoa
dola milioni 800 kwa Tanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo.
Balozi wa Marekani
nchini Tanzania Mhe. Mark Childress aliyekutana na kufanya mazungumzo na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema kutolewa
kwa fedha hizo ni uthibitisho kuwa kutotolewa kwa fedha za awamu ya pili ya
mradi wa changamoto za milenia (MCC-2) hakujaondoa uhusiano na ushirikiano wa
Tanzania na Marekani ikiwemo utoaji wa misaada ya maendeleo.
"Tumezungumza
mambo kadhaa, na wiki hii Tanzania na Marekani kupitia shirika letu la misaada
la USAID tunatarajia kutiliana saini mkataba wa zaidi ya dola milioni 400 kwa
ajili ya mwaka ujao, pia tumezungumza kuwa kutakuwa na dola milioni 800
zitakazotolewa na Marekani kwa ajili ya miradi mbalimbali na hii haihusiani na
MCC.
"Ukweli ni
kwamba tunayo mengi ya kufanya pamoja katika sekta mbalimbali zikiwemo afya,
elimu na kilimo na tutafanya kila juhudi kuhakikisha haya yanafanikiwa" Amesema
Balozi Mark Childress muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo na Rais Magufuli.
Kwa upande wake Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema serikali
yake ya awamu ya tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano
na Marekani na kwamba fedha za msaada kutoka Marekani ni muhimu kwa maendeleo
ya Tanzania.
"Amekuja
kutuhakikishia kwamba watatoa hela kwa ajili ya Tanzania na anasema sasa hivi
watatoa zaidi ya dola milioni 800, na mkataba mwingine tunaweza tukasaini hata
kesho wa dola milioni 410, anasema kutotoa hela za MCC hakuna maana kupotea kwa
urafiki wa Tanzania na Marekani, urafiki wa Tanzania na marekani upo pale pale
na sasa wanaongeza hela nyingi zaidi katika kuonesha kwamba juhudi za HAPA KAZI
TU zinaendelea" amesema Rais Magufuli.
Wakati
huo huo Rais Dkt. John Pombe Magufuli leo amekutana na
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji Mhe. Didier Reynders Ikulu
Jijini Dar es salaam, ambapo viongozi hao wamezungumzia kuendeleza na kuimarisha
uhusiano baina ya nchi hizi mbili hususani katika maendeleo.
Pamoja na
kuzungumzia miradi ya ushirikiano inayotekelezwa kati Tanzania na Ubelgiji katika
mkoa wa Kigoma, viongozi hao pia wamekubaliana kuongeza ushirikiano katika
biashara na uwekezaji ambapo Mhe. Didier Reynders ameahidi kushawishi kampuni
nyingi za Ubelgiji kuja kuwekeza hapa nchini.
Katika
hatua nyingine Rais Magufuli ameagana na Balozi
wa Italia hapa nchini Mheshimiwa Luigi Scotto ambaye amemaliza muda wake wa
miaka mitatu.
Balozi Luigi
Scotto amesema katika kipindi chake amewezesha kuongezeka kwa biashara kati ya
Italy na Tanzania kwa asilimia 35 na ameielezea Tanzania kuwa ni nchi nzuri
aliyoipenda na kwamba ataendelea kutangaza fursa zilizopo Tanzania huko Italia
na kwingineko.
Mapema
leo asubuhi, Rais Dkt. John Pombe Magufuli
ametia saini kitabu cha maombelezo katika Ofisi ya Ubalozi wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Nchi za Kiarabu ya Saharawi iliyopo Mikocheni Jijini Dar es
salaam, kufuatia kifo cha Rais wa nchi hiyo Mohamed Abdelaziz aliyefariki dunia
Jumanne iliyopita tarehe 31 Mei, 2016.
Rais Magufuli
ambaye amepokelewa na Balozi wa Saharawi hapa nchini Mhe. Brahim Salem Buseif
amesema Marehemu Mohamed Abdelaziz ambaye pia alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha
Polisalio Front, atakumbwa kwa juhudi zake za kupigania ukombozi na uhuru wa Saharawi.
"Kwa niaba ya
Serikali na wananchi wa Tanzania napenda kutoa salamu zangu za pole kwa Serikali
na wananchi wa Saharawi kwa kumpoteza kiongozi ambaye alijitoa kwa ajili ya
kupigania ukombozi na uhuru wa Jamhuri ya Saharawi.
"Namuombea
kwa Mwenyezi Mungu, aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina"
Amesema Dkt. Magufuli katika salamu hizo.
0 comments:
Post a Comment