Na Mwandishi wetu, Geita
Masoko ya Madini Katoro na Geita pamoja na vituo vya ununuzi wa madini vinaendelea kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Geita, baada ya kuongeza fursa za ajira, biashara na mzunguko wa fedha katika jamii zinazozunguka maeneo ya shughuli za madini.
Akizungumza kuhusu mchango wa masoko hayo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Mjiolojia Samwel Shoo, amesema uwepo wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini umeimarisha biashara halali ya madini kwa kuweka mfumo wa bei elekezi unaolenga kulinda maslahi ya wachimbaji wadogo na kuongeza uwazi katika biashara ya madini.
Amesema kupitia masoko hayo na vituo vya ununuzi wa madini, wachimbaji wadogo wameweza kuuza madini yao kwa bei nzuri, hali iliyoongeza kipato chao na kuwapa uwezo wa kuboresha maisha yao, ikiwemo kugharamia huduma za kijamii kama elimu, afya na makazi bora.
Mjiolojia Shoo ameongeza kuwa ongezeko la shughuli za masoko ya madini limevutia wafanyabiashara, wasafirishaji na watoa huduma mbalimbali, hatua iliyochochea ukuaji wa biashara ndogondogo, kuongeza ajira kwa vijana na wanawake, pamoja na kuimarisha uchumi wa maeneo yanayozunguka masoko hayo.
Ameeleza kuwa kwa ujumla, Masoko ya Madini Katoro na Geita pamoja na vituo vya ununuzi wa madini yamechangia kuongeza mapato ya Serikali, kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini na kuhimiza maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii katika Mkoa wa Geita.













0 comments:
Post a Comment