Mfungaji wa CDA Dodoma, Tatu Fungo akiuwahi mpira katika
mchezo wao wa netiboli wa Kombe la Mei dhidi ya Uchukuzi SC. Uchukuzi
walishinda kwa magoli 23-16.
Mchezaji Mwadawa Hamisi wa Uchukuzi SC (GK) akiangalia
mwenzake wa kumrushia baada ya Tatu Fungo wa CDA kufunga bao katika michuano ya
Mei Mosi. Uchukuzi walishinda magoli 23-16.
Mchezaji Matalena Mhagama wa Uchukuzi SC (GS)
akijiandaa kupokea mpira kutoka kwa Tatu Kitula aliyezuiwa na Catherine
Ukunguala, katika mchezo wa netiboli wa mashindano ya Mei Mosi.
*****************
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TIMU ya netiboli ya Uchukuzi
SC jana ilianza vyema mchezo wake wa kwanza kwa kuwaicharaza CDA ya Dodoma
katika mashindano ya Mei Mosi yanayoendelea mkoani Dodoma.
Uchukuzi SC inayoundwa na
wachezaji wakongwe, akiwemo mfungaji mahiri wa timu ya Bandari na Taifa,
Matalena Mhagama waliwapeleka puta wapinzani wao ambapo hadi mapumziko walikuwa
mbele kwa magoli 11-6.
Katika mchezo huo uliokuwa
umetawaliwa na rafu za hapa na pale na kulalamikiwa mara kwa mara na wachezaji
wa Uchukuzi SC, ulimalizika kwa mfungaji Matalena kufunga magoli 16 na Tatu
Kitula akifunga saba, wakati wapinzani wao Tatu Fungo nma Margeth Nicholaus
kila mmoja akifunga magoli nane.
Kocha Mkuu wa Uchukuzi SC,
Judith Ilunda alisema wamepata ushindi huo wa kwanza kutokana na kufanya
mazoezi ya pamoja ya muda mrefu, pamoja na kwamba wapinzani wao walikuwa ni
wazuri na wenye uzoefu mkubwa.
“Wengi waliocheza na kikosi
change ni wakongwe wapo niliocheza nao mimi kwenye mashindano mbalimbali, hivyo
wameweza kutumia ukongwe wao lakini tuliwazidi mbinu kutokana na timu yetu
kuundwa na chipukizi wengi,” alisema Ilunda.
Lakini, alilalamikia maamuzi
ya waamuzi waliocheza mchezo huo kuwa mengi yamepitwa na wakati kutokana na
sheria kubadilika mara kwa mara.
“Hawa waamuzi wamekuwa
wakichezeshakwa sheria nyingi za zamani na kusababisha mvutano, hivyo
wanatakiwa wabadilike kwa kujisomea mara kwa mara ili kuondoa mkanganyiko kwa
timu zinazocheza,” alisema Ilunda.
Hatahivyo, waamuzi Mariam Makisi
na Caroline Paulo wote wa Dodoma, kwa nyakati tofauti walisema wamechezesha
mchezo huo kwa kanuni na sheria za mchezo huo, lakini wameshangazwa na
malalamiko ya kuwa wamechezesha kwa sheria za zamani.
“Unajua timu za Dar es Salaam
siku zote zinajifanya kujua sheria zaidi, na wangeweka wazi ni wapi waamuzi
tulipopindisha sheria,” alisema Makisi.
Wakatihuohuo, timu ya Tamisemi
iliwafunga TPDC kwa magoli 6-1 katika mchezo wa soka uliofanyika kwenye uwanja
wa Jamhuri.
Wafungaji wa Tamisemi ni
Mwigane Yeya kafunga magoli mawili, wakati waliofunga moja-moja ni Hamis
Shedafa, Hamad Majura, Nelson Richard na Phillipo Oden; wakati bao la kufutia
machozi la TPDC lilifungwa na Shija Dalushi.
Katika mchezo mwingine wa
soka, timu ya Tanesco ilipata ushindi wa chee baada ya wapinzani wa CWT ya Dodoma
kushindw kutokea uwanjani.
0 comments:
Post a Comment