Ukifika katika kiwada cha Konyangi kilichopo eneo la
Chang’ombe jijini Dar es Salaam na kumkuta Bi.Symphorose Mhanza akiwa mitamboni
huwezi kuamini kama ni mwanamke kutokana na anavyomudu kazi yake ya ufundi na
uendeshaji mitambo.
Symphorose anasema kuwa japo kazi hii inaonekana kuwa ngumu
kwa kuwa kuna wakati inabidi kutumia nguvu nyingi kama ilivyo desturi ya kazi
za ufundi lakini ameizoea na anaipenda.
“Naipenda sana kazi yangu na nimeizoea japo inaonekana kuwa ni ngumu na inafanywa zaidi na wanaume
lakini mimi naona kawaida japo sijaona mwanamke mwingine anayethubutu kuifanya
kiwandani hapa”.Anasema.
Bi.Symphorose anasema
jambo linalompa faraja kubwa na
kuipenda zaidi kazi yake ni kutokana na
jinsi anavyoaminiwa na mabosi wake kiasi kwamba japo ni mwanamke peke yake
katika kiwanda hicho anayefanya kazi hii lakini anathaminiwa na kuaminiwa kama
wanavyoaminiwa wafanyakazi wenzake wanaume.
Akieleza historia yake ya kazi alisema mwanzoni mwa miaka ya
tisini ndipo alipojiunga na kiwada cha Konyagi ambacho hivi sasa kiko chini ya
kampuni ya TBL “Wakati huo ulipokuwa unaajiriwa ulikuwa kwanza unapata mafunzo
ya ndani yaliyokuwa yanatolewa kweye fani mbalimbali ambapo mimi nilijifunza
ufundi na uendeshaji mashine (Machine Operator) kwa kipindi cha mwaka mmoja na
nilipofuzu ndipo nikaanza kuifanya kazi hii”.Anasema.
Bi.Symphorose aliendelea kueleza kuwa baada ya kiwanda hicho
kubinafsishwa kuna mifumo mingi mipya imeanzishwa ikiwemo mafunzo ya mara kwa
mara ambayo anadai yamesaidia kumpatia ujuzi mkubwa katika fani ya ufundi na
uendeshaji mashine na kumjengea uwezo wa kujiamini zaidi.
Alisema anajivunia kufanya kazi katika kampuni hii hasa kwa
jinsi alivyoweza kupata ujuzi mkubwa ambao unamuwezesha kumudu maisha popote
atakapokwenda hata baada ya kustaafu kazi na kuamua kuendesha shughuli zake.
Kuhusiana na changamoto zilizopo katika kazi yake alisema ni
za kawaida kama zilivyo katika kazi nyingine “Changamoto kubwa ni mabadiliko ya
kiteknolojia ambayo ili kwenda nayo
sambamba inabidi uwe na ufuatiliaji wa mambo mbalimbali katika fani ya ufundi
bila hivyo unaweza kuachwa nyuma kwa kuwa kila kukicha inabuniwa mitambo ya
kisasa zaidi”.Alisema.
Kuhusiana na mafanikio ambayo ameyapata kutokana na kazi yake Bi.Symphorose ambaye ni mama wa
familia mwenye mme na watoto anasema
yapo mafanikio kwa kuwa anaweza kuchangia katika pato la familia katika
kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo kusomesha watoto wake.
Mafanikio mengine ni kufundishwa na mwajiri wake mambo mbalimbali
ambayo yanasaidia katika maisha ya kawaida “Hapa tunajifunza usafi wa
mazingira,nidhamu ya kutunza fedha,kupanga bajeti,kuzingatia muda na mambo
mengineyo mengi ambayo yanaweza kukusaidia sehemu yoyote katika maisha na ndio
maana najivunia kufanya kazi kampuni kubwa kama TBL”.Alisema.
Alimalizia kutoa ushauri kwa watanzania wote kuwa tuachane na
uzembe na tufanye kazi kwa bidii popote pale tutakapokuwa tutafanikiwa na pia alishauri wanawake
wenzake kuchangamkia fursa za ajira zitazojitokeza ili kuweza kupata kipato na
kuwakwamua katika janga la umaskini.
0 comments:
Post a Comment