Meneja msaidizi wa kituo cha walemavu cha Usa River
Rehabilitation Centre,Sophia Moshi akibadilishana mawazo na meneja mkuu wa
kituo hicho,Claus Heim.
*************
Mahmoud Ahmad,Arusha
Serikali imeombwa kuchukua
hatua kali kwa baadhi ya wazazi nchini wenye tabia ya kuwaficha watoto wao
wenye ulemavu hali ambayo imekuwa ikiwafanya wakose mahitaji ya msingi kama
elimu na afya.
Ombi hilo limetolewa hivi
karibuni na uongozi wa chuo cha walemavu cha Usa River Rehabilitation
Centre huku wakiiomba serikali iviangalie vituo vya kulea watoto walemavu
kwa kuvipatia ruzuku .
Akizungumza katika mahojiano
maalumu na gazeti hili chuoni hapo,meneja wa chuo hicho,Claus Heim alisema
kwamba serikali inapaswa kuhakikisha inawachukulia hatua kali za kisheria
baadhi ya wazazi wenye tabia ya kuwaficha watoto wao wenye ulemevu majumbani.
Alisema kwamba serikali
inapaswa kuweka sheria kali na kuhakikisha zinatekelezwa ili kuwapa fursa
watoto wenye ulemavu nchini kupata huduma za msingi kama elimu,afya,chakula
pamoja malazi.
“Hawa wazazi wanaowaficha
watoto wenye ulemavu nchini je wanachukuliwa hatua gani?kila mtoto ana haki ya
elimu na afya lakini nani anawajibika”alihoji Heim ambaye ni raia wa nchini
ujerumani
Hatahivyo,meneja msaidizi wa
kituo hicho,Sophia Moshi kwa upande wake alisema kwamba ni wajibu wa serikali
kuhakikisha inavipatia ruzuku vyuo vya ulemavu nchini ili viweze kujiendesha
kwa kuwa vinakabiliwa na changamoto lukuki.
Alisema kwamba mtoto mwenye
ulemavu ana uwezo kama mtoto mwingine na hivyo kuitaka jamii kuwathamini watoto
wenye mahitaji maalumu badala ya kuwanyanyapaa.
Mbali na kauli hiyo Moshi
alisema kwamba chuo chao kimejipanga kujenga shule ya sekondari kwa lengo la
kuongeza mapato ya kuendesha chuo hicho badala ya kutegemea wafadhili ,kusajili
kituo cha afya kwa ajili ya matibabu ya mguu kifundo(club foot) sanjari na
kusajili chuo cha ufundi chuoni hapo.
Chuo hicho kilianzishwa mnamo
mwaka 1988 na kinasimamiwa na kanisa la Kiinjili la Kilutheri(KKKT) Dayosisi ya
Meru ,kwa sasa kina jumla ya wanafunzi 74 walemavu ambao ni wasichana na
wavulana ambapo nchi ya ujerumani ndiye mfadhili mkuu kwa sasa.
0 comments:
Post a Comment