Tanzania imetangaza kufungua
tena ubalozi wake jijini Luanda nchini Angola, hatua inayolenga kuimarisha
uhusiano wa kidiplomasia na kupanua ushirikiano na nchi hiyo katika biashara,
uwekezaji na sekta nyingine za kimkakati.
Uamuzi huo umetangazwa na
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
wakati wa mazungumzo rasmi na Mheshimiwa João Manuel Gonçalves Lourenço, Rais
wa Jamhuri ya Angola, leo, tarehe 29 Oktoba, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Lourenço yuko nchini kwa
ziara ya kitaifa, ikiwa ni ya pili kufanywa na Rais wa Angola tangu ziara ya
Rais wa kwanza na Muasisi wa nchi hiyo, Hayati António Agostinho Neto, mwaka
1979. Akizungumza na waandishi wa habari, Rais Dkt. Samia amesema kiwango cha
biashara kati ya Tanzania na Angola bado ni cha chini licha ya uhusiano wa muda
mrefu na fursa zilizopo katika mataifa yote mawili.
Ili kukuza kiwango cha
biashara, Tanzania imeikaribisha Angola kununua mazao yake ya chakula, huku
ikiona fursa ya kuagiza bidhaa za petroli na mbolea kutoka Angola. Ili
kurahisisha biashara, nchi zote mbili zimekubaliana kuunganisha reli ya
Benguela nchini Angola na TAZARA kupitia Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo, kuwezesha usafirishaji wa mizigo kati ya Bandari ya Lobito katika Bahari
ya Atlantiki na Bandari ya Dar es Salaam katika Bahari ya Hindi.
Kwa upande wa usafiri wa anga,
Rais Dkt. Samia amesema Tanzania na Angola zinalenga kuanzisha safari za ndege
zitakazounganisha nchi hizo bila kupita nchi nyingine.
“Kwa sasa, tunataka kuanzisha
safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Luanda,” amesema Rais Dkt.
Samia.
Katika sekta ya nishati, Rais
Dkt. Samia amesema Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeanza
kutathmini uwezekano wa kuwekeza katika kiwanda cha kusafisha mafuta cha Lobito
nchini Angola.
Nchi hizo pia zimekubaliana
kubadilishana uzoefu katika kuongeza thamani ya madini na kuwajengea uwezo
wataalamu na wachimbaji wadogo, ili waweze kunufaika zaidi na rasilimali hizo.
Kwa upande wake, Rais Lourenço
ametambua mchango wa Tanzania chini ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, katika kusaidia harakati za ukombozi wa Angola zilizoongozwa
na Hayati Dkt. António Agostinho Neto, akisema viongozi wa sasa wana wajibu wa
kuendeleza urafiki huo kwa kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Katika sekta ya afya, amesema
Angola inalenga kuajiri kwa mikataba wataalamu wa afya kutoka Tanzania ili
kukabiliana na upungufu wa watumishi katika hospitali zake zinazoongezeka.
Rais Lourenço amesema nchi
yake itashirikiana na Tanzania katika kubadilishana utaalamu na kutoa mafunzo
kupitia taasisi za elimu ya tiba, pamoja na kuboresha huduma za afya ya mama na
mtoto.
“Hata tuwe na rasilimali
nyingi kiasi gani, hatuwezi kufikia maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi
wetu bila kushirikiana,” amesema Rais Lourenço, akisisitiza umuhimu wa nchi za
Afrika kutumia uwezo uliopo miongoni mwao kukabiliana na changamoto za
maendeleo.
Katika hatua nyingine,
viongozi hao wameshuhudia kusainiwa kwa mikataba na hati za makubaliano ya
ushirikiano katika sekta za anga, mawasiliano na hali ya hewa. Rais Lourenço ataendelea
na ziara yake kesho mkoani Dodoma, ambapo, akiambatana na mwenyeji wake,
atashiriki katika hafla ya uzinduzi wa Majengo ya Ofisi, Wizara na Taasisi za
Serikali, na Barabara za Lami katika Mji wa Serikali Mtumba.
0 comments:
Post a Comment