Na Mwandishi Wetu, BAJP -UDOMWanafunzi wapya wa mwaka wa kwanza wa masomo 2026/2027 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wametakiwa kujikita katika masomo chuoni hapo na kutumia muda na rasilimali fedha kwa weledi ili waweze kutimiza ndoto zao za kitaaluma.
Hayo yamebainishwa na Makamu Mkuu wa Chuo cha UDOM, Prof. Lughano Kusiluka, wakati akizungumza na hadhara hiyo ya wanafunzi wapya wa mwaka wa kwanza katika semina elekezi iliyofanyika katika Ukumbi wa Chimwaga, iliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu mazingira ya Chuo, mifumo ya uendeshaji, taratibu za masomo na mambo muhimu ya kuzingatia katika maisha yao ya elimu ya juu wawapo UDOM.
Prof. Kusiluka amesema kuna mambo mengi ambayo yanapelekea mafanikio kwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu, ambapo amesema nidhamu ya kitaaluma, kupangalia muda na fedha vizuri ili kuweza kufikia mafanikio.
“Kuna vitu vingi vinavyopelekea kufanikiwa kwa mwanafunzi wa Chuo kikuu, hii ni kuanzia na kua na nidhamu ya kitaaluma, kupanga vyema muda wako na namna ya matumizi yako ya fedha, na kuto kufanya hivyo kutapelekea kuanguka na kushindwa kutimima malengo yako,” alisema Prof Kusiluka.
Amesema wanafunzi kama taifa ni mtaji hivyo taifa linawekeza kwao kitaaluma ili nao waweze kuungana na Watanzania wengine katia kuleta maendeleo na kufanya taifa kuwa bora kupitia kile wanachojifunza.
Prof. Kusiluka amewakumbusha wanafunzi hao wanapaswa kuthamini fursa waliyoipata na kuitumia kwa manufaa yao binafsi na jamii kwa ujumla.
“Jikiteni katika masomo yenu, tumieni muda wenu vizuri na fanyeni maamuzi sahihi yatakayowawezesha kufikia malengo yaliyowaleta hapa. Epukeni vitendo na mienendo inayoweza kusababisha kufeli au kuacha masomo kabla ya kuhitimu,” alisisitiza Prof. Kusiluka.
Kuhusu michezo ya kubahatisha, Prof Kusilika amesema si vyema kwa wanafunzi kushiriki michezo hiyo kwani wengi huishia kwenye matumizi mabaya ya fedha za kujikum chuo na ada hivyo kupelekea mwanafunzi kushindwa kusoma kwa umakini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shahada za Awali, Prof. Godlisten Kombe, amewasisitiza wanafunzi hao kuweka kipaumbele katika masomo yao, kuepuka mambo yasiyo na tija yanayoweza kuwatoa katika malengo yao na kuzingatia taratibu za kitaaluma, hususan katika mitihani na masuala ya uongozi.
Semina Elekezi hiyo ni sehemu ya jitihada za Chuo katika kuwaandaa wanafunzi wapya kukabiliana na maisha ya elimu ya juu kwa kuwapatia uelewa kuhusu mifumo ya uendeshaji wa Chuo, uongozi, wajibu wao na fursa mbalimbali zilizopo, ili waanze safari yao ya kitaaluma wakiwa na maarifa na mwelekeo sahihi.
Ndaki zilizoshiriki katika semina hiyo elekezi ya Makamu Mkuu wa Chuo ni pamoja na Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii (CHSS), Ndaki ya Biashara na Uchumi (CoBE), Ndaki ya Sayansi ya Dunia na Uhandisi (CoESE), Ndaki ya Elimu (CoED), Ndaki ya TEHAMA na Elimu Mtandao (CoIVE) na Ndaki ya Sayansi Asilia na Hisabati (CNMS).
Aidha wanafunzi kutoka Shule Kuu ya Sheria (SoL), Shule Kuu ya Tiba na Meno (SoMD) na Shule Kuu ya Uuguzi na Afya ya Jamii (SONPH) nao walishiriki semina hiyo ya Makamu Mkuu wa Chuo.












0 comments:
Post a Comment