Nafasi Ya Matangazo

October 28, 2026

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameiagiza Wizara ya Nishati kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kuandaa mpango mkakati wa kuwajengea uwezo vijana na kampuni za Kitanzania ili washiriki kikamilifu katika miradi ya mafuta na gesi asilia.

Ametoa maelekezo hayo leo, Oktoba 28, 2026, jijini Dar es Salaam, katika hafla ya utiaji saini leseni za utafutaji wa mafuta na gesi.

Katika hafla hiyo, Makamu wa Rais alimwita mbele kijana Mwizegwa Rusibamanyila, aliyeacha kazi nje ya nchi na kurudi nyumbani kuanzisha kampuni yake inayofanya kazi katika kitalu cha gesi cha Mnazi Bay, mkoani Mtwara. Kampuni hiyo imeajiri zaidi ya Watanzania 50, na asilimia 80 kati yao wanatoka katika kijiji kinachozunguka mradi huo. Miongoni mwao ni binti aliyeajiriwa akiwa bado mwanafunzi, akaendelezwa kielimu, na sasa ni mmoja wa wasimamizi wa mradi huo.

“Kitengo cha local content tukikisimamia vizuri, tuna uwezo wa kuzalisha akina Rusibamanyila wengi zaidi ambao watakuja kuajiri Watanzania wenzao katika miradi ya mafuta na gesi,” amesema Mhe. Ndejembi.

Amesisitiza kuwa maandalizi ya vijana hao yaanze sasa, kabla miradi mikubwa ikiwemo mradi wa LNG mkoani Lindi haijakamilika, ili Watanzania wawe tayari kushiriki kama wataalamu, watoa huduma na wasambazaji wa bidhaa.

Aidha, amemshauri Waziri wa Nishati kuandaa tuzo maalum kwa kijana huyo kutokana na kazi kubwa anayoifanya.
Posted by MROKI On Wednesday, October 28, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo