Mwandishi wa habari na mtangazaji wa Radio Free Africa William Bundala maarufu kwa jina la “kijukuu cha bibi k”
**********
Siku moja tu baada ya Tume ya
Uchaguzi nchini Tanzania kutangaza majimbo mapya ya Uchaguzi,Mwandishi wa
habari na mtangazaji wa Radio Free Africa William Bundala maarufu kwa jina la
“Kijukuu cha Bibi K” ametangaza rasmi kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania
Ubunge katika Jimbo la jipya la Ushetu katika halmashauri ya wilaya ya Ushetu
mkoani Shinyanga,kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA.
Bundala ametangaza kuingia kwenye mchakato wa kugombea kuteuliwa na Chama ili aweze kupeperusha bendara ya Chadema/UKAWA katika uchaguzi mkuu ujao katika mkutano wake wa kutangaza nia uliofanyika katika Kijiji cha Bogomba “B” kata ya Ubagwe wilayani Kahama.
Mtia nia huyo alisema endapo Chama chake kitampitisha na hatimaye kushinda Ubunge katika Jimbo hilo atahakikisha anasukuma kasi ya maendeleo katika jimbo hilo jipya lenye Rasimali nyingi kupitia nafasi yake na wajibu kama anavyotakiwa Mbunge Kufanya.
Alisema kuwa dhamira yake imemsuta kwenda kuwatumikia wananchi wa wilaya hiyo ambayo yeye ni mzawa na kuwa atahakikisha anapigania maendeleo ya wananchi kwa kasi huku akiondoa uonevu kwa waandishi wa habari na watumishi wengine serikalini na katika halmashauri za wilaya.
Sambamba na hayo amesema kuwa sababu nyingine iliyomsukuma ni kuona wagombea wengine wanaolitaka jimbo hilo hawako kwa ajili ya ukombozi wa jimbo hilo bali wako kwa ajili ya maslahi binafsi kutokana na asilimia kubwa ya wagombea hao si wakazi wa eneo hilo na kwamba hawafahamu matatizo ya wana ushetu kama anavyoyafahamu yeye.
Aliongeza kuwa akifanikiwa kuukwaa Ubunge pia atasimamia kuhakikisha Jimbo hilo jipya linapata Chuo cha ufundi kwa ajili ya vijana wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne kupata elimu jambo lilatalopunguza wimbi la ukosefu wa ajira kwa vijana.
Bundala alisema kipaumbele kingine atakachoshughulikia ni pamoja na kusimamia na kutoa elimu ya Sheria kupitia wanasheria ambao watazunguka katika kata kutoa elimu hiyo hususan katika maswala ya umiliki wa Ardhi,Mirathi,haki za wakulima na wafugaji pamoja na haki za raia na mali zao kwa ujumla.
0 comments:
Post a Comment