Miaka karibu 16 sasa baada ya kuuawa kwa mwandishi wa habari za
uchunguzi wa nchini Burkina Faso, Norbert Zongo, hatimaye haki imetendeka juu
yake baada ya hukumu ya kihistoria iliyotolewa na Mahakama ya Afrika ya Haki za
Binadamu na Watu (ACHPR) yenye makao yake jijini Arusha. Anaandika
Mtuwa Salira wa EANA-Arusha.
Mtuwa Salira wa EANA-Arusha.
Katika hukumu hiyo iliyotolewa mwishoni mwa wiki, ACHPR iliamuru
Burkina Faso kuifungua na kuisikiliza upya kesi hiyo iliyohusisha pia mauaji ya
watu wengine watatu.
Hukumu hiyo iliyosomwa karibu kwa muda wa saa moja mbele ya jopo la
majaji 10 lilokuwa likiongozwa na Jaji Kiongozi, Gerard Niyungeko, ilimuru pia
serikali ya Burkina Faso kuchukua jukumu la kuwasaka na kuwapata watuhumiwa wa
mauaji hayo.
Mahakama hiyo iliielekeza serikali ya Burkina Faso kuhakikisha kufanya
kila linalowezekana kuwafikisha watuhumiwa husika kwenye vyombo vya sheria ili
nao wapate haki wanayostahili kisheria.
Serikali ya Burkina Faso ilifunga jalada la kesi hiyo mwaka 2006 kwa
maelezo ya kukosa ushahidi.
Mahakama pia imeamuru serikali ya nchi hiyo kuzilipa fidia ya zaidi ya
dola za Marekani milioni 1, familia za watu hao waliouawa.
Inadaiwa kwamba Zongo aliuawa akiwa na wenzake hao watatu alipokuwa
anafanya harakati za kuandika habari za uchunguzi wa dereva wa kaka yake Rais
aliyepinduliwa wa Burkina Faso, Blaise Compaore mwaka 1998.
Mwandishi huyo wa habari za uchunguzi na Mhariri wa gazeti la kila wiki
la L’Independent na wenzake walipatikana wakiwa wamechomwa moto hadi kufa
wakiwa katika gari yao karibu kilometa zipatazo 100 kutoka makao makuu ya nchi
hiyo, Ouagadougou.
0 comments:
Post a Comment