Wataalam
wa Sekta ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Shirika
la Umeme nchini (Tanesco), wakiongozwa na Kamishna Msaidizi wa Umeme
Mhandisi Innocent Luoga (wa kwanza kushoto), wakiwa katika mazungumzo na
wawakilishi wa Kampuni ya Sunshine Group Ltd (Kulia). Mazungumzo
yalifanyika hivi karibuni Makao Makuu ya Wizara, jijini Dar es Salaam na
yalihusu uanzishwaji wa Kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme za zege
kwa ajili ya kusambaza umeme nchini.
Ujumbe
kutoka Kampuni ya Sunshine Group Ltd, ukiwa katika mazungumzo na
wataalam wa Sekta ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na
Shirika la Umeme nchini – Tanesco (hawapo pichani). Kampuni hiyo
iliwasilisha mapendekezo (proposal) ya kuanzisha Kiwanda cha kutengeneza
nguzo za umeme za zege kwa ajili ya matumizi ya hapa nchini.
Kamishna
Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga (Kulia) akimsikiliza
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Sunshine Group Ltd, Bw. Sun Tao aliyekuwa
akitoa ufafanuzi wa jambo fulani, mara baada ya kumalizika kwa
mazungumzo baina ya Wataalam wa Wizara na wawakilishi wa Kampuni hiyo
kuhusu uwezekano wa kuanzisha Kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme za
zege kwa ajili ya kusambaza umeme nchini.
*******
Na Veronica Simba
Serikali
inaendeleza jitihada za kuachana na matumizi ya nguzo za umeme za miti
na badala yake kutumia nguzo za zege ikiwa ni hatua mojawapo ya
kuboresha huduma ya usambazaji na upatikanaji wa umeme nchini.
Hayo
yalibainika mwishoni mwa wiki katika kikao baina ya uongozi wa Kampuni
ya Sunshine Group Ltd na wataalam wa sekta ya umeme kutoka Wizara ya
Nishati na Madini pamoja na Shirika la Umeme nchini (Tanesco).
Katika
kikao hicho, Kampuni ya Sunshine iliwasilisha mapendekezo (proposal) ya
kuanzisha kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme za zege kwa ajili ya
matumizi ya hapa nchini.
Akieleza
msimamo wa Serikali kuhusu mapendekezo hayo, Kamishna Msaidizi wa
Umeme, Mhandisi Innocent Luoga alisema Serikali ina dhamira ya kutumia
nguzo za umeme zilizotengenezwa kwa zege na kuachana na za miti
zinazotumika sasa kutokana na manufaa yake.
Mhandisi
Luoga aliyataja manufaa ya kutumia nguzo za zege kuwa ni pamoja na
uimara wa nguzo husika. “Huwezi kulinganisha uimara wa nguzo za zege na
hizi za miti tunazotumia hivi sasa. Nguzo za zege ni madhubuti na imara
zaidi,” alisema.
Akifafanua
zaidi, Mhandisi Luoga alisema, kutokana na uimara wa nguzo za zege,
uhai wake ni wa muda mrefu kulinganisha na nguzo za miti.
“Uhai
wa nguzo za zege ni kati ya miaka 70 hadi 100, wakati uhai wa nguzo za
miti ni miaka 50,” alisema Luoga na kusisitiza kuwa sifa hiyo ya uhai
mrefu wa nguzo za zege inazalisha manufaa mengine kwa Serikali na
wananchi kwa ujumla endapo nguzo hizo zitatumika.
Akielezea
manufaa yanayotokana na uhai mrefu wa nguzo za zege, Mhandisi Luoga
alisema Serikali itatumia fedha kidogo kutokana na nguzo za zege kudumu
kwa muda mrefu, tofauti na nguzo za miti ambazo uhai wake ni mdogo.
Aidha,
faida nyingine za kutumia nguzo za zege, zilizotajwa na wataalam katika
kikao hicho ni pamoja na kuwa rafiki wa mazingira ambapo huepusha
ukataji wa miti.
Nyingine
ni uwezo wake wa kutopitisha maji na kutoshika moto kwa urahisi (water
and fire proof). Akihitimisha mazungumzo husika, Kamishna Luoga alisema
Serikali itaendelea kufanya mazungumzo na Kampuni hiyo pamoja na
wawekezaji wengine wenye nia ya kutengeneza nguzo za umeme za zege ili
kufikia makubaliano yatakayowezesha pande zote mbili kunufaika.
“Mkakati
wetu ni kwa Tanesco kutengeneza nguzo za zege kwa matumizi ya ndani ya
nchi lakini ni vema tukapata wawekezaji wengine watakaosaidia
kutengeneza nguzo hizo kwani mahitaji ni makubwa sana,” alisema.
0 comments:
Post a Comment