Nafasi Ya Matangazo

November 11, 2013

Ndugu Wanahabari,
NILIPOKUWA katika ziara ya bara la Ulaya kati ya Oktoba 21 mpaka Novemba 2 mwaka huu (2013), nilipokea kwa njia ya barua pepe ripoti inayoitwa "Taarifa ya Siri ya Chadema" ambayo pia ilikuwa imesambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
 “Taarifa ya Chadema inasema kwamba chama hicho (chama changu) kilikuwa kimechunguza mwenendo wangu tangu mwaka 2008 hadi 2010 na kubaini kuwa mimi napokea fedha kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga Chadema.
 
Ripoti hiyo ilinihusisha pia na mwananchi raia wa Ujerumani, Andrea Cordes ambaye, kwa mujibu wa ripoti hiyo, alinisaidia kupokea na kuhifadhi kiasi cha dola 250,000 za Marekani kupitia kwenye akaunti yake binafsi.
 
Taarifa hii ya kutunga na iliyojaa uongo wa kiwango cha kutisha, imenifadhaisha, kunisikitisha na kunikasirisha.
 
Taarifa hii iliibuliwa katika kipindi ambacho nilikuwa safarini kutetea haki za Watanzania na Waafrika ambao utajiri wao wa rasilimali unafaidiwa na watu wachache waliohifadhi mali katika nje za nje na pia kupigania makampuni ya mataifa tajiri yalipe kodi stahiki katika nchi zetu.
 
Pengine lengo la ripoti hiyo lilikuwa ni kutaka kunipoteza kutoka katika nia na dhamira yangu ya dhati ya kutaka Watanzania wafaidike na utajiri wao. Muda ambao watunzi wa ripoti hiyo waliamua kutoa taarifa yao unazua maswali mengi kuliko majibu.
 
Nafahamu kwamba mimi ni mwanasiasa ambaye nimekuwa mlengwa (target) wa mashambulizi kutoka kwa makundi mbalimbali ya wanasiasa na vikundi vyao. Kama mwanasiasa, niko tayari kupokea changamoto zozote zinazokuja na uanasiasa wangu.

Hata hivyo, ambacho sitakubali ni kwa watu kutumia jina langu na uanasiasa wangu kunichafua mimi binafsi na watu wengine wasiohusika kwa sababu ya kutaka kutimiza malengo yao ya kidhalimu.
 
Raia huyo wa Kijerumani tayari amekana kuhifadhi fedha zangu. Kwa maelezo yake kwa baadhi ya viongozi wa Chadema amekana kuwa na akaunti inayotajwa na amekana pia kuwepo nchini Ujerumani katika siku na wakati uliotajwa kwenye ripoti hiyo.
 
Ripoti hiyo imemtaja pia mtu kama Dk. Charles Kimei, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB ikidai kwamba nilikutana naye na alishiriki kwenye igizo hilo la kunipa fedha.

Niseme mapema kwamba tangu kuzaliwa kwangu sijawahi hata mara moja kukutana na Dk. Kimei popote pale ndani au nje ya nchi. Kumuingiza mtu ambaye amejenga jina lake kwenye taaluma ya kibenki kwa sababu tu ya lengo ovu la kumchafua Zitto Zuberi Kabwe si uungwana bali ni unyama.

Kutokana na uchafuzi huu wa wazi dhidi ya taswira yangu binafsi na watu wengine walioingizwa kwenye mkumbo huu, nimeandika rasmi kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Wilbrod Slaa kumwomba athibitishe kwamba kinachoitwa Taarifa ya Siri ya Chadema ni kweli ni taarifa ya chama au kiikanushe ili niweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waandishi wa hekaya hiyo.
 
Cha ajabu, nimepokea ujumbe wa kutishiwa maisha kutoka kwa mtu anayejiita Theo Mutahaba na kuahidiwa KUPOTEZWA endapo nitaendelea na jitihada zangu za kupambana na ufisadi na kutafuta haki kwa Watanzania wote pasipo kujali tofauti zao za kiitikadi, kikanda, kikabila na kidini.
 
Natarajia kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote ambao wamehusika na utungaji na uenezi wa taarifa hii. Nitahakikisha kwamba wahusika wanatafutwa na kufunguliwa mashitaka stahiki ya upotoshaji na kuchafuana.
 
Ni matarajio yangu kwamba wale wenye mapenzi mema na Tanzania, mimi binafsi na utawala wa sheria, wataelewa nia yangu ya kutafuta haki katika suala hili.
Nimeamua kujitolea maisha yangu kwa ajili ya Watanzania na kama alivyopata kusema Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela; “Struggle Is My Life.”
 
Forward Ever, Backward Never- Kwame Nkrumah
 
Zitto Kabwe (Mb)
10/11/2013
Posted by MROKI On Monday, November 11, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo