USAJILI wa mbio za Uhuru Marathon,
ulioanza kwa kishindo wiki iliyopita pale Spika wa Bunge, Anne Makinda
alipowaongoza wabunge kufanya hivyo, unazidi kushika kasi huku
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications, Tido Mhando (pichani)
naye akiahidi kujisajili leo ili aweze kushiriki.
Kampuni hiyo ni wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na gazeti la michezo la
Mwanaspoti.
Akizungumza
na gazeti hili jana, Katibu wa Kamati ya Uhuru Marathon, Innocent
Melleck alisema, Tido anatarajiwa kujisajili kushiriki mbio hizo, baada
ya kuvutiwa na lengo lake ambalo ni kuimarisha amani, umoja na
mshikamano.
Melleck
hakutaka kufafanua Tido anataka kushiriki mbio za kilomita ngapi,
ingawa alisema zitatolewa kwa Sh 100,000 kwa wale watakaokimbia mbio za
kilomita tatu, Sh 2,000 mbio za kilomita tano, Sh 6,000 kwa
atakayeshiriki moja kati ya mbio za kilomita 21 au 42.
“Hizi mbio ni muhimu zaidi kwa ajili ya Taifa letu, hivyo ni vyema kwa Watanzania wote wakashiriki ili
kuipigania amani iliyopo nchini mwetu na ndiyo maana hata Rais Jakaya Kikwete, pia atashiriki.
“Kesho
(leo) Tido anatarajiwa pia kujisajili kwa ajili ya kushiriki mbio hizo,
lengo kubwa ikiwa pia kushawishi Watanzania wengine waweze kushiriki,”
alisema.
Mratibu
huyo alisema mbio za kilomita 3 zitakuwa maalumu kwa ajili ya viongozi
wa kada mbalimbali, wakiwemo pia wale wa dini na zile za kilomita 5 pia
zitakuwa za kuchangia kwa ajili ya watu wa mahitaji maalumu.
“Hapa
tunachotaka kufanya katika mbio za kilomita 3 mbali na Rais Kikwete,
pia tunawaomba viongozi maarufu wa dini mbalimbali pamoja
na viongozi wetu kada nyingine kushiriki, kwa kudumisha amani na
upendo.
“Pia
tutahakikisha kama mbio za kilomita 5, zinakuwa kwa ajili ya kuchangia
watu wenye mahitaji maalumu na tayari tuna uhakika mkubwa wa wanariadha
maarufu zaidi duniani kushiriki,” alisema.
Mbio
hizo zinatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam hapo Desemba 8, mwaka
huu na zitaanzia na kuishia katika Viwanja vya Leaders vilivyopo
Kinondoni.
0 comments:
Post a Comment