JAJI Steven Ihema na wakili
mwandamizi, Bi. Jesse Mguto wataongoza kamati muhimu za za maadili za
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zilizoundwa baada ya kufanya
mabadiliko kwenye katiba ya Shirikisho hilo mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais
wa TFF Leodegar C. Tenga alitangaza jana.
Shirikisho hilo pia limemteua
Jaji Bernard Luanda kuongoza Kamati ya Rufaa za Uchaguzi wakati Profesa Mgongo
Fimbo ataendelea kuongoza Kamati ya Rufaa za Nidhamu na Kamanda Mstaafu, Alfred
Tibaigana akiendelea kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu.
Rais Tenga alisema hayo wakati
alipoongea na waandishi wa habari jana kwenye ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa
Taifa mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Utendaji, ambacho
kikatiba kina jukumu la kuunda Kamati Ndogo za TFF na vyombo vya maamuzi.
“Tulitaka tuwe na watu solid
(imara) na makini ambao watatuhakikishia tunakwenda vyema,” alisema Tenga
akizungumzia uteuzi huo ambao unahitimisha mchakato wa mageuzi kwenye
Shirikisho baada ya Uchaguzi Mkuu wa TFF uliopangwa kufanyika mwezi Februari
kusimamishwa kutokana na baadhi ya wagombea kupinga kuenguliwa na baadaye
kwenda FIFA.
Katika kumaliza tatizo hilo,
FIFA ilituma ujumbe wake kusikiliza walalamikaji na watu wengine na baadaye
kuagiza kuundwa kwa Kamati za Maadili na kufanyika kwa Mkutano Mkuu Maalum wa
TFF kwa ajili ya kuingiza vyombo hivyo kwenye katiba kabla ya kuelekea kwenye
Uchaguzi Mkuu wa TFF.
“Tumezingatia pia maoni ya
wajumbe wa Mkutano Mkuu ambao walitaka kamati ziwe na majaji... lakini si
rahisi kupata seating judges (majaji walio kazini) ndio maana tunawashukuru
wale waliotuambia kuwa wako tayari kutusaidia.
“Tumetafuta majaji na mawakili
waandamizi ambao tunaamini watatuhakikishia haki inatendeka na inaonekana
inatendeka,” alisema Tenga na kuongeza kuwa pia walizingatia maombi ya wajumbe
wengine watatu ambao walitaka kupumzika, akiwataja kuwa ni Deo Lyatto,
Sylvester Faya na Idd Mtiginjollah.
Alisema kutokana na mfumo huo
mpya, mambo yote yanayohusu masuala ya ndani ya uwanja sasa yatashughulikiwa na
Kamati ya Nidhamu, wakati yale ya nje ya uwanja, ambayo yanawahusu viongozi na
wanafamilia ya mpira wa miguu kwa ujumla, yatashughulikiwa na Kamati za
Maadili.
Tenga alisema mabadiliko hayo
pia yamegusa kamati nyingine mbili, yaani Kamati ya Nidhamu na Kamati ya
Uchaguzi ambayo sasa itaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Zanzibar,
Hamidu Mbwezeleni
Jaji Ihema ataongoza Kamati ya
Rufaa za Maadili akisaidiwa na mwanasheria mwingine mwandamizi, Victoria
Makani, huku Bi. Mguto, ambaye anakuwa mwanamke wa kwanza kuongoza vyombo vya
vya maamuzi ataongoza Kamati ya Maadili akisaidiwa na makamu wake Francis
Kabwe, ambaye Msajili wa Mahakama Kuu.
Katika uteuzi huo, baadhi ya
wajumbe wamehamishwa kutoka kamati moja hadi nyingine. Mhe. Murtaza Mangungu,
ambaye awali alikuwa Kamati ya Rufaa za Uchaguzi, sasa ataingia kwenye Kamati
ya Rufaa za Maadili; Kamanda Mohamed Mpinga na Prof Madundo Mtambo wamehamishwa
kutoka Kamati ya Rufaa za Uchaguzi kwenda Kamati ya Maadili.
Wajumbe wapya kwenye Kamati
hizo ni pamoja na kocha wa zamani wa Taifa Stars na Reli ya Morogoro, Mshindo
Msolla na Kamanda Mstaafu Jamal Rwambow wanaingia kwenye Kamati ya Nidhamu;
mwanasheria maarufu Evodi Mmanda anaingia kwenye Kamati ya Maadili; mwanasheria
mwandamizi Mustapha Kambona ambaye anaingia kwenye Kamati ya Nidhamu; Mhe.
Mohamed Misanga ambaye anaingia kwenye Kamati ya Maadili na Kanali Iddi
Kipingu, ambaye anasifika kwa kuendesha soka la vijana, anaingia kwenye Kamati
ya Rufaa za Nidhamu.
Pia Mwanasheria Anne Steven
Marealle anakuwa mjumbe kwenye Kamati ya Rufaa za Uchaguzi; Yohane Masale
(Rufaa za Uchaguzi), Allen Kasamala (Rufaa za Uchaguzi); Francis Kiwanga
ambaye pia aningia kwenye Kamati ya Rufaa za Uchaguzi na mkufunzi wa FIFA,
Henry Tandau ambaye anaingia kwenye Kamati ya Rufaa za Maadili.
Kamati ya Utendaji pia
imefanya mabadiliko kwenye Kamati ya Waamuzi ambako mwenyekiti Said Nassoro na
katibu Charles Ndagala wa Chama cha Waamuzi wanaingia kwenye kamati hiyo
kushika nafasi ya Joan Minja na Riziki Majala.
Wajumbe wa Kamati hizo ni kama
ifuatavyo:
Kamati ya Rufaa za Maadili ni
Jaji Steven Ihema (mwenyekiti), Victoria Makani (m/mwenyekiti), Mhe. Mohamed
Misanga, Henry Tandau na Mhe. Murtaza Mangungu.
Kamati ya Maadili: Bi Jesse
Mguto (mwenyekiti), Francis Kabwe (m/mwenyekiti), ACP Mohamed Mpinga, Prof.
Madundo Mtambo, na Evod Mmanda.
Kamati ya Rufaa za Nidhamu:
Prof. Mgongo Fimbo, Ong’wanuhama Kibuta (m/mwenyekiti), Kanali Mstaafu Idd
Kipingu, Dk. Mshindo Msolla, ACP Jamal Rwambow.
Kamati ya Nidhamu: Kamanda
Mstaafu Alfred Tibaigana (mwenyekiti), Mustafa Kambona (m/mwenyekiti), Azzan
Zungu, Yussu Nzowa na Mohamed Msomali.
Kamati ya Rufaa za Uchaguzi:
Jaji Bernard Luanda (mwenyekiti), Francis Kiwanga (m/mwenyekiti), A. Steven
Semu, Yohane Masalla na Allen Kasamala.
Kamati ya Uchaguzi: Hamidu
Mbwezeleni (mwenyekiti), Moses Kaluwa (m/mwenyekiti), Mustafa Siani, Hassan
Dyamwale na Kitwana Manara.
Kamati ya Waamuzi: Kapteni
Mstaafu Stanley Lugenge (mwenyekiti), Omar Kasinde (m/mwenyekiti), Said
Nassoro, Charles Ndagala na Mohamed Nyama.
0 comments:
Post a Comment