NnnMkuu wa Wilaya ya Kiteto akagua miradi ya elimu yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.37
Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mhe. Remidius Mwema,tarehe 17 Agosti 2026 alifanya ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali katika sekta ya elimu yenye thamani ya jumla ya Shilingi bilioni 1.37, katika Kata za Partimbo, Engusero na Laiseri.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mwema pia alizungumza na wananchi kwa kusikiliza na kutatua kero mbalimbali,akiwa katika Kata ya Laiseri, Mhe. Mwema alishuhudia mapokezi makubwa na bashasha kutoka kwa wananchi kufuatia hatua ya Serikali kutegua kitendawili cha muda mrefu cha ukosefu wa shule ya sekondari katika kata hiyo.
Serikali tayari imeanza ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari Laiseri, ambayo itakuwa shule ya kwanza ya sekondari katika kata hiyo.Mapema akizungumza na wananchi, Mhe. Mwema alisema:
_“Serikali imekata kiu kwa wananchi wa Kata ya Laiseri kufuatia hitaji la shule ya sekondari. Tambueni kwamba vijiji na kata zote zina usawa kimtazamo linapokuja suala la maendeleo ya wananchi, sasa Serikali imetekeleza kwa vitendo. Wito wetu kwenu ni kuendelea kutoa ushirikiano katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi huu,”Alisema.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mwema alitembelea na kukagua maendeleo ya miradi ifuatayo:
Ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari Mbeli – Kata ya Partimbo, wenye thamani ya Shilingi milioni 584.
Ujenzi wa Bweni katika Shule ya Sekondari Engusero, wenye thamani ya Shilingi milioni 204.
Ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari Laiseri, wenye thamani ya Shilingi milioni 584.
Miradi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha wananchi wa maeneo yote wanapata huduma bora za elimu.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya amesema hakuna Kijiji au kata ambayo inasahaulika linapokuja suala la maendeleo, Ujenzi wa Sekondari Laiseri ilikuwa ni hitaji muhimu na muda mrefu kwa wananchi wa kata Laiseri, leo Serikali imetekeleza hitaji hili kubwa na itaendelea kugusa maisha ya Wananchi wote Wilayani Kiteto.













0 comments:
Post a Comment