Nafasi Ya Matangazo

July 24, 2013

Katibu Mtendaji toka Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) Rehema Twalib akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu mpango wa Serikali kuanza utekelezaji wa ripoti ya APRM,kwenye mkutano uliofanyika leo ukumbi wa Idara ya Habari, kulia ni Afisa Habari na Mawasiliano wa APRM Hassan Abbas.
*********
Tumewaita leo kuwapa mrejesho ninyi kama wadau wa APRM lakini pia muwafikishie wananchi kwa ujumla taarifa hii muhimu kuhusu hatua zilizofikiwa na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kujitathmini Kiutawala Bora chini ya APRM.

Kama mnavyofahamu Tanzania ni miongoni mwa nchi 33 sasa kati ya 54 za Umoja wa Afrika zilizosaini Mkataba wa kutekeleza mpango huu wa APRM unaolenga kutathmini hali ya utawala bora kwa kuwashirikisha wananchi kuzishauri Serikali zao ili kupata maendeleo endelevu nay a pamoja.

Tanzania imekamilisha zoezi hili la kwanza na la aina yake kwa nchi yetu na tayari Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete aliiwasilisha Ripoti ya Tanzania na kujadiliwa mbele ya viongozi wenzake wa Umoja wa Afrika Januari 26 mwaka huu jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Katika wasilisho hilo, Tanzania ilipongezwa kwa hatua kadhaa ilizofikia katika kuimarisha utawala bora na vile vile Serikali ilipewa muda wa kufanyiakazi maeneo yenye changamoto.

Kwa mujibu wa Mkataba wa APRM sasa nchi yetu, inatakiwa kuanza kutekeleza Mpangokazi wa Kitaifa wa miaka minne (NPoA) unaolenga kufanyiakazi maeneo anuai yaliyobainishwa kuwa na changamoto ambayo kimsingi ni maoni ya wananchi.Taarifa za utekelezaji zitatolewa kila mwaka. Tathmini ya APRM hurudiwa kila baada ya miaka minne ya utekelezaji wa NPoA.


                                    KALENDA YA UTEKELEZAJI
 Tunapenda kuwaarifu rasmi kuwa pamoja na kwamba Ripoti hii itazinduliwa rasmi Oktoba mwaka huu, tayari Serikali ya Tanzania imeonesha dhamira ya dhati kwa kuanza utekelezaji wa maoni ya wananchi kama ifuatavyo:-

1.      Baadhi ya masuala yaliyoainishwa na yanayohusu Katiba yaliwasilishwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba na mengi yameingizwa kwenye rasimu iliyotolewa hivi karibuni;

2.      Baadhi ya Masuala yameingizwa kwenye mfumo wa Mpango wa Mwaka na Bajeti iliyopitishwa hivi karibuni ya 2013/14;

3.      Baada ya uzinduzi mwezi Oktoba, masuala mengine yote yaliyosalia yataingizwa katika Mipango na Bajeti za miaka ijayo za wizara na taasisi nyingine husika.

4.      APRM Tanzania itaendelea kusimamia utekelezaji na kuripoti kwa umma. Tathmini ya utawala bora itarudiwa tena kila baada ya miaka minne.

Asanteni kwa kutusikiliza na kuipokea taarifa hii na kwa mchango wenu jadidi katika kutangaza shughuli za APRM Tanzania.

Imetolewa na:

 HASSAN ABBAS,
AFISA HABARI NA MAWASILIANO,
APRM TANZANIA.
Posted by MROKI On Wednesday, July 24, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo