WENYEVITI WA FA NDIYO WASIMAMIZI RCL
Wakati
mechi za kwanza za raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL)
zinachezwa wikiendi hii, Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) imesisitiza kuwa wasimamizi wa mechi za ligi hiyo
ni wenyeviti wa mikoa wa vyama vya mpira wa miguu.
Kamati
hiyo chini ya uenyekiti wa Ramadhan Nassib ilikutana jana (Mei 23 mwaka
huu) kupitia ripoti za makamishna kwa mechi za raundi ya kwanza ya RCL
iliyomalizika wikiendi ya Mei 18 na 19 mwaka huu.
Kuhusu
viwanja vinavyotumika kwa ligi hiyo, Kamati imesema vitaendelea kuwa
vile vya makao makuu ya mikoa, na kwa vile vilivyokuwa vimeombwa
vifanyiwe marekebisho ili viweze kukaguliwa kwa ajili ya RCL msimu ujao.
Pia imeitaka mikoa kuendelea kuboresha viwanja vinavyotumika sasa,
lakini vina upungufu.
Vilevile
Kamati imebaini kuwa zimekuwepo pingamizi kuhusu usajili wa wachezaji
ambapo imesema haiwezi kujadili pingamizi hizo kwa vile mikoa yote
haikuwasilisha usajili wa wachezaji wa klabu husika uliofanyika mikoani
kama ilivyoagizwa na kuelekezwa na TFF.
Hata hivyo, Kamati imeitaka mikoa ambayo klabu zao zimefanikiwa kuingia raundi ya pili kuwasilisha usajili huo haraka.
Pia
Kamati imebaini kuwa zipo baadhi ya klabu ambazo zimekata rufani kuhusu
usajili wa baadhi ya wachezaji, na kusisitiza kilichowasilishwa ni
pingamizi kwa vile kwa mujibu wa kanuni masuala ya uwanjani hayakatiwi
rufani. Hivyo, Kamati imeshauri klabu zilizokata rufani zilirejeshewe
ada zilizolipa kwa ajili hiyo.
Makamishna
na waamuzi wanaosimamia mechi za RCL wamekumbushwa kuwa ili mchezaji
aruhusiwe kucheza mechi ni lazima awe na leseni yake (kadi ya usajili),
vinginevyo asiruhusiwe kucheza mechi husika.
Mechi
za RCL zinaendelea wikiendi hii ambapo zote zitachezwa Jumapili (Mei 26
mwaka huu) isipokuwa mechi kati ya Friends Rangers ya Dar es Salaam na
African Sports ya Tanga itakayochezwa Jumamosi (Mei 25 mwaka huu) kwenye
Uwanja wa Azam ulioko Chamazi.
Nayo
mechi kati ya Abajalo ya Dar es Salaam na Kariakoo ya Lindi iliyokuwa
ichezwe Jumamosi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam
sasa itachezwa Jumapili kwa vile siku hiyo uwanja huo utatumika kwa
mazoezi ya Taifa Stars.
Mechi
nyingine za RCL zitakazochezwa Mei 26 mwaka huu ni Machava FC ya
Kilimanjaro dhidi ya Mpwapwa Stars ya Dodoma kwenye Uwanja wa Ushirika
mjini Moshi, Stand United FC ya Shinyanga itakuwa mgeni wa Magic
Pressure ya Singida kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.
Polisi
Jamii ya Bunda mkoani Mara na Biharamulo FC ya Kagera zitaumana kwenye
Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma. Mjini Kigoma kwenye Uwanja
wa Lake Tanganyika ni kati ya wenyeji Saigon FC na Katavi Warriors ya
Katavi.
Nayo
Kimondo SC ya Mbeya itakuwa mgeni wa Njombe Mji ya Njombe katika mechi
itakayochezwa Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe. Mechi za marudiano
zitachezwa kati ya Juni 1 na 2 mwaka huu.
Timu
zitakazofuzu kucheza raundi ya tatu zitacheza mechi za kwanza kati ya
Juni 8 na 9 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitakuwa kati ya Juni 15
na 16 mwaka huu.
SEMINA YA USAJILI- TMS KUFANYIKA MEI 25
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeandaa semina ya usajili kwa njia
ya mtandao (Transfer Matching System-TMS) kwa klabu za Ligi Kuu ya
Vodacom kwa ajili ya msimu wa 2013/2014.
Semina
hiyo itafanyika Jumamosi (Mei 25 mwaka huu) kwenye ofisi za TFF saa 3
kamili asubuhi ikishirikisha watu wawili kutoka kila klabu ambao ni TMS
Manager, na ofisa mwingine wa klabu.
Klabu
za ligi hiyo zinazotakiwa kuhudhuria semina ya usajili ni Ashanti
United, Azam, Coastal Union, JKT Ruvu, Kagera Sugar, Mbeya City, Mgambo
Shooting, Mtibwa Sugar, Oljoro JKT, Rhino Rangers, Ruvu Shooting, Simba,
Tanzania Prisons na Yanga.
0 comments:
Post a Comment