Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kina uhakika wa
kushinda katika Uchaguzi Mkuu ujayo wa mwaka 2015 kutokana na kwamba bado kipo
imara na kinakubalika na Watanzania wengi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Ndugu NAPE NNAUYE wakati akizungumza na
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Tawi la Ofisi Ndogo Makao Makuu na baadhi ya wanachama
wa Tawi hilo mara baada ya kufungua Ofisi Mpya ya Tawi la Ofisi Ndogo.
Kwa imani hiyo amesema hakuna sababu ya Wana-CCM
kukata tamaa kwani wamezunguka Mikoani na kujionea hali halisi ya jinsi
wananchi wanavyoendelea kukiamini Chama tawala ambacho ni Chama cha Wakulima na
Wanyonge.
Kuhusu migongano ya Dini Katibu huyo wa NEC,
Itikadi na Uenezi amesisitiza kuwa migongano hiyo itamalizwa na Chama kwa
kushirikiana na viongozi na wananchi kwani CCM ndicho Chama pekee chenye
kudumisha amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Mapema akisoma risala ya wanachama wa Tawi la
CCM la Ofisi Ndogo ya Makao Makuu lililopo katika Kata ya Jangwani, Katibu wa
Tawi Ndugu ROSE THOMAS amesifu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na chama katika
kurejesha imani ya CCM kwa wananchi.
Tawi hilo la Ofisi Ndogo lina Mashina Sita na
lina wanachama 308.
0 comments:
Post a Comment