Ndugu
waandishi wa habari, baadhi yenu mnafahamu kuwa Baraza la Vijana la
Chadema Taifa (BAVICHA), limefanya kikao cha kawaida cha Kamati Tendaji,
juzi 5 Januari 2013, katika Hotel ya Benzi Garden jijini Dar es Salaam,
ambapo pamoja na mambo mengine, kilijadili masuala matatu mazito.
Kwanza, Kamati Tendaji ilijadili kwa kina suala la kuporomoka kwa elimu
nchini, ambapo serikali imepunguza alama za viwango vya kufaulu, jambo
ambalo limesababisha mamia ya wanafunzi waliochaguliwa kutokuwa na sifa.
Pili, Kamati Tendaji ilijadili jinsi Bavicha itakavyoshiriki katika
maandilizi ya utekelezaji wa maazimio ya Kamati Kuu ya Chadema
yalioeleza kuwa mwaka 2013 ni mwaka wa nguvu ya umma.
Tatu, Kamati Tendaji ilijadili kwa kina “Tuhuma za usaliti na njama za
kuvuruga chama, kutukana viongozi wakuu wa chama na kuvuruga wanachama
wa Chadema na Baraza kwa ujumla.”
Ndugu waandishi wa habari, yapo baadhi ya vyombo vya habari jana na leo
vimeripoti kwa upotoshaji mkubwa wa baadhi ya masuala yaliyojadiliwa na
kikao hicho.
Kwa mfano, gazeti moja la kila siku limemtaja mwanachama wetu mmoja kuwa
ndiye aliyekuwa mtoa taarifa wetu muhimu na kusema mbunge mmoja wa
CHADEMA alijadiliwa katika kikao hicho kuwa ni miongoni mwa kundi hili
la MASALIA na kufika mbali zaidi kwa kusema, “…sasa amekalia kuti kavu.”
Lakini ukweli wa kilichojadiliwa kikaoni ni huu ambao tunaueleza sasa:
Kwanza, kuhusu ajenda ya kuporomoka kwa elimu: Kamati Tendaji imeagiza
kuwa utafiti uliofanywa na BAVICHA katika ngazi ya sekondari, ambao
umegundua madudu mbalimbali, uongezwe hadi shule za Msingi na taarifa
yake ililetwe kwenye kikao kijacho cha Kamati Tendaji.
Kwenye ajenda ya pili: Kamati ya Utendaji BAVICHA, ilipokea na kujadili
agizo la Kamati Kuu ya Chama iliyoeleza kuwa mwaka 2013 ni mwaka wa
nguvu ya umma.
Katika ajenda ya tatu juu ya tuhuma za usaliti na njama za kuvuruga
chama, kutukana viongozi wakuu wa chama na kuvuruga wanachama wa
CHADEMA, na Baraza, Kamati ya Utendaji ilipokea taarifa ya Kamati Ndogo
ya Kamati Tendaji iliyoundwa Septemba mwaka jana kwenye kikao chake
kilichofanyika mjini Morogoro. Kamati ilipewa muda wa mwezi mmoja
kukamilisha kazi hii.
Katika hili, watuhumiwa wakuu walikuwa ni kama ifuatavyo:
- Juliana Shonza, Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa
- Habib Mchange, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA
- Mtela Mwampamba, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA
- Gwakisa Burton Mwakasendo, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA
- Joseph Kasambala, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA
Aidha, baada ya Kamati iliyoundwa kuwahoji baadhi ya watuhumiwa na
wanachama wengine mbalimbali, ilibaini kwamba wapo baadhi ya wanachama
wa BAVICHA ambao wameshiriki kwa namna moja au nyingine katika tuhuma
hizi. Hao ni pamoja na Ben Saanane – maarufu kama Eight Oclock.
Katika orodha hiyo, wakatajwa pia Exaud Mamuya lakini kamati ikashindwa
kumpata Mamuya kwa kuwa hakukuwa na mawasiliano ya kutosha.
Ndugu waandishi wa habari, hizi sasa ni tuhuma za kila mmoja:
Ndugu Juliana Shonza:
Alituhumiwa akiwa katika nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA,
amekuwa akishirikiana na baadhi ya watu kupanga njama na kufanya usaliti
dhidi ya Baraza, Chama na vijana wenzake wapenda mabadiliko nchini.
Amekuwa akifanya mikutano na vikao vya siri, kwa manufaa ya CCM,
akiwakusanya vijana wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali waliosimamishwa
masomo au kufukuzwa vyuoni kwa kutimiza wajibu wao wa kudai haki zao za
msingi na uwajibikaji wa serikali na ambao ni wanachama wa CHASO.
Juliana alifanya kazi yake hiyo kwa ushawishi wa hongo, ili wakubali
kuitisha mkutano na waandishi wa habari, watoe matamko machafu dhidi ya
CHADEMA na viongozi wake wakuu, akiwamo Dk. Willibrod Slaa na Freeman
Mbowe.
Mfano dhahiri hapa ni kikao alichofanya Baa ya Highland iliyoko maeneo
ya Makumbusho, majira ya saa 9 hadi saa 11, ambapo aliwaita viongozi wa
CHASO, akawashawishi kuwa watakuwa na maisha mazuri, watarudishwa vyuoni
na kutunzwa vizuri hapa mjini kama anavyoishi yeye, endapo tu
watakubali kufanya press conferences na kuisema CHADEMA kuwa inawavuruga
vijana walioko vyuoni.
Tarehe 6, Desemba, 2012 Hotel MIC, kuanzia saa 10 hadi saa 12, aliwaita
baadhi ya vijana ambapo yeye na wenzake walipanga njama za kukichafua
chama na kutukana viongozi, kwa manufaa ya CCM.
Ifuatayo hapa chini ni moja ya sms ambazo Juliana Shonza alikuwa
akiwaandikia vijana katika ushawishi wake wa usaliti kwa mapambano haya
ambayo chama chetu kinafanya, kuwapigania Watanzania maskini na wanyonge
katika nchi yao;
“jembe chukua bodaboda basi jamaa washatia timu hela yako yakulinda
mfuko wako utaikuta tumempa eddo mnaetoa naye tamko tutalindana tu jembe
usijali.”
Huu ni moja tu kati ya ushahidi mwingi, wa meseji, simu, sauti, video,
picha na vikao kadhaa katika maeneo mbalimbali, unaomwingiza Shonza na
wenzake wengine katika sifa mbaya ya usaliti wa chama, baraza na
viongozi wake na wanachama wenzao na umma wa Watanzania kwa ujumla.
Hapo alikuwa akimwandikia mmoja wa viongozi wetu ili ashiriki katika
press conference ambayo yeye Makamu Mwenyekiti kwa kushirikiana na
wenzake wengine, walikuwa wameiandaa kwa nia ya kuchafua chama,
kulichafua baraza, kutukana viongozi waandamizi pamoja na kuvuruga na
kuchonganisha wanachama wa CHADEMA.
Matokeo ya kikao hicho cha MIC Hotel, yalionekana siku moja baada ya
kikao hicho, ambapo mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Edo Mwamalala,
aliyeshiriki kikao hicho cha MIC Hotel, aliitisha mkutano na waandishi
wa habari, akijitambulisha kuwa ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CHADEMA,
cheo ambacho hakuwa nacho.
Aidha, Shonza amekuwa akikutana na kufanya vikao vya siri na wenzake,
wakipanga njama za kufanya kazi na majukumu ya CCM kuhujumu BAVICHA
pamoja na CHADEMA. Mikakati ya kuvuruga baraza, kuchonganisha wanachama
na kutukana chama na viongozi wakuu, kwa siri na hadharani, imekuwa
ikipangwa katika vikao hivi.
Amebainika kukiuka kipengele cha 10.1(x) cha Maadili ya Viongozi, cha
Katiba toleo la mwaka 2006, kinachomtaka kiongozi yeyote asitoe tuhuma
zozote juu ya viongozi wenzake pasipo kupitia vikao halali, kwa
kuzingatia taratibu na kanuni za chama.
Ameonesha ubaguzi wa kikabila na kikanda kupitia maandiko yake kwenye
mtandao kwa kutumia jina lake, anapungukiwa na sifa muhimu na mahsusi za
kuwa kiongozi, kwa mujibu wa kipengele cha 10.1(iv) kinachomtaka
kiongozi yeyote asijihusishe na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini
au ukanda vinavyolenga kuleta ubaguzi ndani ya chama.
Kwa kushiriki vikao vya kuanzisha chama kipya kinachoitwa CHAUMMA,
kushiriki katika makundi yaitwayo MASALIA na PM7 ambayo yote yalikuwa na
lengo la kuvuruga chama na wanachama, kukosanisha na kutukana viongozi
wa chama, ndugu Shonza amevunja kipengele cha 10.1(i),(viii)(ix) na
ibara ya 10.2(iv).
Kwa kushiriki vikundi hivyo hapo juu, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya
BAVICHA wamejiridhisha pasi na shaka kuwa Shonza haendani na katiba,
falsafa, sera na maadili ya chama makini na tumaini la watu, CHADEMA.
Hivyo kwa mujibu wa ibara ya 5.1.4 na 5.1.5 anakosa sifa za kuwa
mwanachama wa Baraza la Chama.
Kwa kutoa tuhuma za uongo dhidi ya wanachama na viongozi wenzake,
ameendelea kuvunja kanuni za uendeshaji kazi za chama ibara ya
10.1(viii).
Amehusika katika kuanzisha, kujihusisha na kuratibu moja kwa moja kundi
la vijana waliokuwa wakizunguka mikoani na kushawishi viongozi wa vijana
kutoa matamko kwa kutumia jina la CHADEMA kufanya kazi na majukumu ya
CCM ya kukichafua chama, kugombanisha wanachama na kumtukana Katibu Mkuu
kwa kutumia propaganda za CCM.
Kamati Ndogo ilimuita Ndugu Shonza ili kumhoji. Lakini aligoma kwa madai
kuwa haitambui kamati hiyo na wala hajui kuwa kuna mgogoro, jambo
ambalo limetushangaza wengi kwa kuwa Ndugu Shonza alikuwapo katika kikao
cha Morogoro kilichounda Kamati hii.
Ndugu Shonza pia hakuhudhuria kikao cha Kamati Tendaji cha juzi kwa
madai kuwa amebanwa na shughuli za familia. Baada ya kupitia maelezo
yote hayo, Kamati Tendaji iliamua yafuatayo:
Ndugu Juliana Shonza, amepoteza sifa na uhalali wa kuwa mwanachama wa
Chadema kwa kukiuka ibara ya 5.3.4 na ibara ya 10.1(ix) ya katiba ya
CHADEMA na hivyo imeamua kumuondoa katika nafasi yake ya makamu
mwenyekiti na kumfuta uwanachama wake.
Hivyo basi, kwa maamuzi hayo ya Kikao cha Kamati ya Utendaji ya BAVICHA,
kuanzia juzi tarehe 5 Januari 2013, Ndugu Juliana Shonza, si mwanachama
wa BAVICHA na hivyo moja kwa moja amepoteza sifa za kuwa kiongozi wa
baraza na kwa nafasi yake aliyokuwa nayo ya Makamu Mwenyekiti Tanzania
Bara.
Habib Mchange:
Huyu alituhumiwa kutoa tuhuma za uongo, zikiwemo za mauaji, kinyume na
maadili ya Wanachama (kipengele cha 10.3(3); kuunda vikundi
vinavyojulikana kwa majina ya MASALIA na PM7 – Pindua Mbowe.
Pia Ndugu Mchange alituhumiwa kuwavuruga wanachama, kuwachonganisha na
kuwatukana viongozi, kisha kushiriki vikao vya kuanzisha chama kingine
cha siasa cha CHAUMMA.
Alituhumiwa pia kupotosha maamuzi halali ya vikao vya chama na Baraza hivyo kuendelea kukipaka chama matope.
Kamati ilimuita Mchange, na kumhoji juu ya tuhuma zinazomkabili.
Hakufika. Badala yake, aliandika barua kueleza kuwa hana imani na
kamati:
Aidha, pamoja na Mchange kugoma kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Kamati
Tendaji, Sekretarieti ya Kamati Tendaji Taifa, ilimuita Ndugu Mchange
kuhudhudhuria mkutano wa Kamati Tendaji ili kujibu tuhuma
zinazomkabili.
Mwaliko huu ulifanywa kwa njia ya barua na simu. Njia hizo ndio
zilizotumika kualika wahusika wote wakiwamo wajumbe wa Kamati Tendaji,
Ndugu waandishi wa habari, baadhi yenu mnafahamu kwamba Ndugu Mchange
alikuwa miongoni mwa wanachama wa BAVICHA waliotaka kuwania nafasi ya
uenyekiti wa taifa wa baraza hili. Jina lake liliondolewa na Kamati Kuu
ya CHADEMA, kutokana na kukosa maadili ya uongozi.
Kamati Tendaji baada ya kusikiliza hoja yake hii, ikajiridhisha kuwa
mtuhumiwa ameamua kuibuka hoja hiyo ili kutaka Kamati Tendaji isimjadili
ili aendeleze mradi wake wa kukichafua chama akiwa ndani ya chama.
Hivyo Kamati Tendaji imefanya yafuatayo: Imempata na hatia ya kuvunja
ibara ya 10.3(iii) na kwenda kinyume na kanuni za uendeshaji wa chama
ibara ya 10.3(4), kinyume na Maadili ya Wanachama (kipengele cha
10.3(3); uendeshaji wa chama ibara ya 10.3(4) na kwamba mambo yote haya
yanadhihirisha kuwa Ndugu Mchange hayuko tayari kushirikiana na viongozi
wake kama mwanachama, hivyo kukiuka katiba ya chama ibara ya 5.3.4 na
kuafikiwa uamuzi wa kumfukuza uwanachama wa Bavicha na Chadema.
Mtela Mwampamba:
Huyu ametuhumiwa kutoa tuhuma nzito za uongo hadharani, zikiwemo za
mauaji, kinyume kabisa na Maadili ya Wanachama (kipengele 10.3(3).
Kuvunja katiba ya chama ibara ya 5.3.4 na Kanuni za Uendeshaji kazi za
chama Ibara ya 10.3(4) kwa kupotosha maamuzi halali ya vikao vya chama
na baraza na kukipaka matope chama pamoja na kudhihirisha kuwa hayuko
tayari kushirikiana na viongozi wake kama mwanachama.
3.Amevunja Katiba ya CHADEMA ibara ya 5.3.3 na 5.3.4 kwa kutoa kauli za
kichochezi dhidi ya chama, kuwachonganisha wanachama na kuwatukana
viongozi.
4.Kwa kujiunga na vikundi vinavyoitwa MASALIA NA PM7 na baadae kushiriki
vikao vya kuanzisha chama cha CHAUMMA, Ndugu Mwampamba amevunja ibara
ya 10.3(iii).
5.Kinyume na ibara ya 5.3.3 na 5.3.4 ya Katiba ya CHADEMA na Ibara ya
4.3(g) na (i) ya kanuni za BAVICHA, zinazopinga ubaguzi wa aina yoyote
ile, Ndugu Mwampamba ameonesha hisia za ubaguzi wa kikabila na kikanda.
Gwakisa Burton Mwakasendo:
Huyu amekuja kwenye kikao na kukiri kutenda makosa yake ambayo takriban
yote ni sawa yanayowahusu watuhumiwa waliotangulia hapo juu. Mbele ya
kikao cha Kamati ya Utendaji alikiri kushiriki vikao, akisema kuwa
‘lakini’ alilazimika ‘kuikimbia’ dhambi kwa kuondoka katika baadhi ya
mikutano na watu hao, wakati mwingine hata nyumbani kwake hakuweza
kulala akihisi ‘dhambi’ hiyo anayoikimbia itamfuata nyumbani.
Kamati Tendaji, iliamua kumpa adhabu ya kuwekwa chini ya uangalizi kwa
mwaka mzima, katika wakati wote huo amezuiwa kugombea nafasi yoyote
ndani ya BAVICHA na onyo kali la barua.
Ben Saanane:
Huyu pamoja na kwamba hakuwa miongoni mwa watuhumiwa alipewa adhabu ya
onyo kali na uangalizi wa miezi 12, kutokana na makosa yafuatayo. Kutoa
tuhuma nzito, zinazomhusu pia Kiongozi wa juu mwandamizi wa chama, Ben
amekiuka Maadili ya Wanachama (kipengele 10.3(3).
Kukiri kuwa mmoja wa waanzilishi wa vikundi vinavyoitwa MASALIA na PM7
na kisha kushiriki vikao vya kuanzisha chama kingine cha CHAUMMA,
amevunja ibara ya 10.3(iii), kwa nia ya kuvuruga chama na kutukana
viongozi wake:
Mbele ya Kamati Tendaji, Ben alikiri makosa na akaomba radhi.
Aidha, Ben alitoa ushirikiano mkubwa kwa Kamati Ndogo jinsi ya
kupatikana kwa taarifa na ushahidi wa namna wanachama wa BAVICHA
walivyokuwa wanafanya kazi za kundi hili la MASALIA na PM 7 na hasa juu
ya majina wanayotumia katika mitandao mbalimbali ya kijamii, wakifanya
juhudi za kuivuruga CHADEMA, kuvuruga BAVICHA, kutukana viongozi na
kuwavuruga wanachama, lakini kikubwa wakionesha kila dalili ya tabia ya
usaliti.
Exaud Mamuya:
Huyu hajapata nafasi ya kusikilizwa kwenye vikao. Hivyo suala lake litaendelea kufanyiwa kazi na uongozi wa BAVICHA.
Aidha, kikao cha Kamati ya Utendaji pia kilipitisha kwa kauli moja, moja
ya maazimio ya BAVICHA Mkoa wa Mwanza, waliopendekeza kufukuzwa
uanachama kwa aliyekuwa Katibu wa Mkoa wa Mwanza, Salvatory Magafu, kwa
tuhuma za kukiuka Kanuni ya 10.1(xii) kwa kutoa tamko kwenye vyombo vya
habari kwa nia ya kumfarakanisha Katibu Mkuu na wanachama wa CHADEMA na
umma wa Watanzania, ikiwa ni sehemu ya uratibu wa kundi lililokuwa
likiendeshwa na watuhumiwa wengine hapo juu.
Kamati ya Utendaji pia ilimkuta na makosa ya kiuongozi katika tuhuma
zilizowasilishwa vikaoni na kufanyiwa kazi na Kamati Ndogo, Mwenyekiti
wa Vijana Mkoa wa Mbeya, Joseph Kasambala na hivyo amepewa adhabu ya
onyo kali.
Hitimisho
Tunaomba kuwahakikishia vijana wenzetu wa CHADEMA na wengine wote
wapenda mabadiliko nchini, hakuna kijana mwanachama wa BAVICHA, atafanya
kazi za kuhujumu baraza na chama kwa ujumla na kusaliti matumaini pekee
ya Watanzania, akifanya kazi za mahasimu wetu, kisha akaachwa.
Ni lazima na muhimu tuoneshe kuwa tuna uthubutu kwa kuchukua hatua kadri
inavyotakiwa, pale panapotakiwa. Tuliopewa dhamana za uongozi,
tutatimiza wajibu kuhakikisha hakuna mtu ataonewa wala kupunjwa haki
yake katika kusimamia utendaji na utoaji utumishi bora wa baraza kwa
wanachama wake na chama kwa ujumla.
Daima tutasimamia katiba ya chama, maadili, kanuni, taratibu, itifaki na
miongozo ya mabaraza. Baraza hili halitakuwa tayari kuwa sehemu ya
kuruga matumaini makubwa ya Watanzania waliyonayo juu ya CHADEMA.
Baraza liko imara. Wanachama wetu wasifadhaishwe na upotoshaji
unaofanywa na wasaliti kuwa tumevurugika au ‘kumechafuka’. Hatuwezi
kuchafuka wala kuvurugika kwa kuchukua maamuzi dhidi ya watu wabinafsi
wanaotaka kukwamisha mapambano ya awamu ya pili, kupigania mabadiliko ya
kweli ya kimfumo na kiutawala, kwa ajili ya Watanzania.
Historia inatuonesha kuwa mara zote ambapo mapambano yamefikia hatua ya
juu ya kutimiza malengo, ndipo ambapo wasaliti hujitokeza. Hivyo vikwazo
hivi vya baadhi yetu kuanza kugeuka nyuma ni dalili za mwisho mwisho
kuwa ushindi unakaribia. Ni lazima kama vijana tuendelee kujenga imani
na matumaini ya Watanzania waliyonayo juu ya CHADEMA kutukabidhi dola
mwaka 2015.
Mwisho
Imetolewa leo Januari 7, 2013, Dar es Salaam na;
John Heche
Mwenyekiti wa Taifa,
Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA)
0 comments:
Post a Comment